Wananchi wa Buhongwa Wajitolea Kujenga Upya Kituo cha Polisi Kilichochomwa Moto


 Wananchi wa Kata ya Buhongwa na kata jirani ya Lwanhima, Wilaya ya Nyamagana mkoani Mwanza, wamejitolea kukijenga upya Kituo cha Polisi Buhongwa kilichochomwa moto wakati wa vurugu za Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025.


​Hatua hiyo imekuja baada ya wananchi hao kupata adha ya kutafuta huduma za kipolisi kwa kusafiri umbali mrefu. Awali, kituo hicho kilikuwa kinatoa huduma kwa wananchi zaidi ya 200,000 wa kata hizo mbili na kata jirani ya Mkolani kabla hakijaharibiwa.

​Akitoa taarifa kuhusu adha ya kukosa kituo cha polisi na kuwaombea msamaha watu waliochoma kituo hicho wakati wa vurugu zilizotokana na Uchaguzi Mkuu wa mwaka jana, Diwani wa Kata ya Buhongwa, Mhandisi Anderson Mfinanga, amesema vijana waliofanya uhalifu huo tayari wamejifunza na wamemtuma awaombee msamaha.


​"Kwa mateso tuliyopitia tangu kituo chetu kilipochomwa moto, sasa wamesema 'mateso sasa basi' na wako tayari kushirikiana na Jeshi la Polisi kurejesha huduma ya Jeshi la Polisi," amesema Mhandisi Mfinanga.


​"Tayari wananchi wameanza kujitolea na tumeanza kuleta malighafi za ujenzi ili huduma irejee. Naamini leo tutaondoka na jibu la pamoja ili huduma hii muhimu irejee," alisisitiza Mfinanga.


​Katika hatua nyingine, Mhandisi Mfinanga amempongeza Polisi Kata wa kata hiyo, Mkaguzi wa Polisi Clemence Masululi, kwa namna anavyoihudumia kata hiyo yenye mitaa 18 pamoja na changamoto zake, licha ya kukosa kituo cha polisi.

Akizungumza na wananchi hao Juni 22, 2026 katika mkutano wa hadhara eneo la Buhongwa kilipochomwa kituo hicho, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, DCP Wilbrod Mutafungwa, ameridhia ombi la wananchi wa kata hiyo la kukijenga upya kituo hicho kwa nguvu zao huku akiwataka kujitafakari kwa kile kilichotokea na kusababisha uharibifu huo.


​"Sawa tunawasamehe, lakini hamna budi tutafakari ni kitu gani kiliwapeleka pale hadi kituo cha polisi kikachomwa moto na si kituo tu, bali mali za watu binafsi na ofisi nyingine za Serikali ziliharibiwa," amesema Kamanda Mutafungwa.


​Pamoja na kuridhia ombi la wananchi la kurejeshwa kwa kituo hicho, Kamanda Mutafungwa amewasisitiza kuendelea kujitafakari kwa kutunza amani ya nchi ili yale yaliyojitokeza yasijirudie tena.


​"Ndugu zangu, tunatakiwa tutafakari kwa kina. Tukishatafakari, tuseme hivi kwa pamoja, wakazi wa eneo hili na wakazi wa maeneo mengine kwamba tusiruhusu tena vitendo vya vurugu na uvunjifu wa amani katika maeneo yetu," alisema.


Makundi mbalimbali, wakiwemo wafanyabiashara, wameunga mkono juhudi hizo ili kuhakikisha ujenzi wa kituo hicho unaanza na huduma hiyo inasogea karibu.
​"Hata wafanyabiashara tunapata adha kubwa sana baada ya kituo cha polisi kuchomwa moto," amesema Mahiri Chacha.

​"Tumepata shida tangu kituo hiki kilipochomwa moto; ukimwona mtu mnapishana naye, unataka kukimbia kwa sababu tunakuwa tuna hofu. Tunawasihi wasirudie kufanya jambo kama hili," amesema Zaidi Harub.

​Zaidi ya fedha taslimu shilingi milioni 5 zimechangwa na wananchi, mifuko 74 ya saruji na matofali Pc 1,200 vimetolewa wakati wa mkutano huo wa hadhara, ambapo makadirio ya gharama za ujenzi wa kituo hicho ni zaidi ya shilingi milioni 30 hadi kukamilika kwake.


Na Pascal kadushi
Post a Comment (0)
Previous Post Next Post