Jeshi la Polisi Mkoa wa Mwanza limewafikisha mahakamani watu wawili wakituhumiwa kwa makosa ya jinai yanayohusiana na dawa za kulevya.
Washtakiwa hao, Madumuka Zilihona (60) na Mawazo Manisha (50), wote wakiwa ni wakulima na wakazi wa kijiji cha Busekeseke wilayani Sengerema, walipandishwa kizimbani Jumanne, Juni 23, 2026, katika Mahakama ya Wilaya ya Sengerema ambapo mmoja amesomewa mashtaka mawili na mwingine shtaka moja.
Mshtakiwa wa kwanza, Madumuka Zilihona, amesomewa makosa mawili mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi, Magreth Maruma. Kesi hiyo iliendeshwa na Wakili wa Serikali, Rivona Kasinisala, akisaidiwa na Wakili Joel Moses.
Kosa la Kwanza ni Kukutwa na dawa za kulevya kinyume na Kifungu namba 15 (1)(a) na (3)(iii) cha Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Dawa za Kulevya, Sura ya 95 Marejeo ya mwaka 2023, ikisomwa pamoja na aya ya 23 ya jedwali la kwanza na vifungu vya 57(1) na 61(2) vya Sheria ya Udhibiti wa Makosa ya Uhujumu Uchumi na Uhalifu wa Kupangwa (Economic and Organized Crime Control Act), Sura ya 200 (Marejeo ya mwaka 2023).
Mshtakiwa huyo hakutakiwa kujibu chochote mahakamani hapo kwani mahakama hiyo haina mamlaka kisheria kusikiliza shauri hilo la uhujumu uchumi.

"Mahakama hii haina mamlaka ya kusikiliza shauri hili, kwa hiyo hutatakiwa kujibu chochote juu ya tuhuma zinazokukabili. Vilevile, kosa la kwanza linalokukabili halina dhamana kisheria, hivyo utaendelea kubaki mahabusu hadi pale upelelezi utakapokamilika," alisema Hakimu Maruma.
Kosa la Pili ni Kulima mimea isiyoruhusiwa kinyume na Kifungu namba 11(1)(a) na (d) cha Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Dawa za Kulevya Sura ya 95 toleo la mwaka 2023.
"Madumuka Zilihona, mnamo tarehe 23 Mei 2026, katika Kata ya Kalebezo iliyopo Wilaya ya Sengerema, Mkoa wa Mwanza, ulikutwa umelima ekari mbili za mimea isiyoruhusiwa (bangi)," alieleza Wakili Rivona wakati akisoma hati ya mashtaka.
Kwa upande wa mshtakiwa wa pili, Mawazo Manisha, amesomewa shtaka moja mbele ya Hakimu Magreth Maruma na wakili wa serikali Rivona Kasinisala akisaidiwa na mawakili wawili, Elisha Hamsini na Joel Moses katika kesi namba 14196 ya Mwaka 2026, ambapo anadaiwa kutenda kosa la kukutwa na dawa za kulevya kinyume na Kifungu namba 16(1) na (2)(c) cha Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Dawa za Kulevya, Sura ya 95 toleo la mwaka 2023.
"Mawazo Manisha, mnamo tarehe 23 Mei 2026, katika Kitongoji cha Nyerere Road kilichopo Kijiji cha Busekeseke, Wilaya ya Sengerema, Mkoa wa Mwanza, ulikutwa na dawa za kulevya aina ya bangi yenye uzito wa kilo 13.50," alisema Wakili Rivona.
Mshtakiwa huyo alikana shtaka hilo. Hakimu Maruma alieleza kuwa kosa hilo lina dhamana na kuweka masharti kwamba mshtakiwa anapaswa kuwa na wadhamini wawili watakaosaini dhamana (bondi) ya Shilingi milioni 4 kila mmoja, kuwa na vitambulisho vinavyotambulika, pamoja na barua za utambulisho kutoka Serikali za Mitaa. Hata hivyo, mshtakiwa alishindwa kukidhi vigezo hivyo vya dhamana kwa siku ya leo.
Kesi zote mbili zimeahirishwa hadi Julai 2, 2026, na washtakiwa wote wawili wamerudishwa rumande.