Alpha Ni Nyenzo Muhimu ya Kuwafikia Vijana Wanaotafuta Majibu ya Maisha na Imani'' Dr. Daniel Mwangili

 

Skywave Tv

Mkurugenzi wa Alpha Tanzania, Dr. Daniel Mwangili, amesema kuwa Alpha ni nyenzo muhimu sana katika kuwafikia vijana mbalimbali ndani ya jamii na makanisa ambao wanakabiliwa na maswali mengi kuhusu maisha, kusudi la kuishi, imani na changamoto zinazowakabili katika dunia ya sasa.


Dr. Mwangili ametoa kauli hiyo wakati wa Kongamano la Alpha Tanzania lililofanyika jijini Dar es Salaam, likiwakutanisha viongozi wa dini, wachungaji, watumishi wa Mungu na washiriki mbalimbali kutoka maeneo tofauti ya Tanzania na nje ya nchi.


Akizungumza katika kongamano hilo, Dr. Mwangili alisema kuwa vijana wengi wa kizazi cha sasa wanahitaji mazingira salama ya kuuliza maswali, kujadili changamoto zao na kupata majibu yanayowasaidia kujenga msingi imara wa maisha na imani. Alisema Kozi ya Alpha imeendelea kuwa jukwaa muhimu linalowawezesha vijana hao kufanya mazungumzo ya wazi kuhusu masuala ya kiroho na maisha kwa ujumla.


“Vijana wengi wana maswali makubwa kuhusu utambulisho wao, kusudi la maisha, mahusiano, imani na mustakabali wao. Alpha inatoa nafasi ya kipekee ya kusikiliza, kujifunza na kujadili masuala hayo kwa uhuru na heshima,” alisema Dr. Mwangili.


Kongamano hilo lilihudhuriwa na viongozi mbalimbali wa madhehebu tofauti ya Kikristo, huku mgeni rasmi akiwa Apostle Vernon Fernandes, ambaye ni Mwenyekiti wa Makanisa ya Kipentekoste Tanzania. Pia kongamano hilo lilihudhuriwa na Askofu Dr. Magnus Muhiche, ambaye ni Makamu Askofu Mkuu wa Tanzania Assemblies of God (TAG).


Akizungumza katika kongamano hilo, Apostle Vernon Fernandes alisisitiza umuhimu wa Kanisa kuendelea kubuni njia mpya za kuwafikia vijana na makundi mengine ya jamii kwa kutumia mbinu zinazowezesha mazungumzo, ushirikishwaji na uinjilisti wa kisasa unaoendana na mahitaji ya wakati huu.


Kwa upande wake, Askofu Dr. Magnus Muhiche aliipongeza Alpha Tanzania kwa juhudi zake za kuunganisha makanisa na viongozi wa Kikristo katika lengo la pamoja la kuifikia jamii kwa Injili ya Yesu Kristo, akisema kuwa programu za Alpha zimekuwa chachu ya kuimarisha uinjilisti, uanafunzi na ukuaji wa kiroho katika makanisa mengi.


Kongamano hilo lilihitimishwa kwa wito kwa makanisa, taasisi za Kikristo na viongozi wa dini kuendelea kutumia Kozi ya Alpha kama nyenzo ya kuwafikia watu wa rika mbalimbali, hususan vijana, ili kuwasaidia kupata majibu ya maswali yao na kujenga mahusiano ya karibu na Mungu pamoja na jamii inayowazunguka.


Na Pascal Kadushi

Post a Comment (0)
Previous Post Next Post