Ligi inayowahusisha watoa huduma wa sherehe mbalimbali ikiwemo Ma-DJ, Ma-MC na Ma-Director inatarajiwa kuanza rasmi tarehe 25 Februari 2026 katika Uwanja wa Isamilo International School, jijini Mwanza. Mashindano hayo yataanza saa moja usiku na yanatarajiwa kukutanisha washiriki na wadau mbalimbali wa tasnia ya burudani kutoka maeneo tofauti.
Akizungumza kuhusu maandalizi ya ligi hiyo, mmoja wa wakurugenzi wa mashindano hayo, Bwana Haiper, amesema kuwa lengo ni kuinua vipaji na kutoa fursa kwa watoa huduma kuonesha uwezo wao mbele ya hadhira kubwa. Ameeleza kuwa maandalizi yamekamilika na kila kitu kiko tayari kwa uzinduzi huo.
Kwa mujibu wa waandaaji, mshindi wa msimu huu ataondoka na zawadi ya ng’ombe, jambo linaloongeza hamasa na ushindani miongoni mwa washiriki. Wadau wa burudani jijini Mwanza na maeneo ya jirani wamehimizwa kujitokeza kwa wingi kushuhudia tukio hilo muhimu.
