NIPE TITLE NZURI YA KUVUTIA 'Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe. Said Mtanda amesema Skimu ya Taifa ya Hifadhi ya Jamii kwa Sekta Isiyo Rasmi (NISS) iliyoboreshwa inalenga kuwafikia Watanzania wengi waliojiajiri ili wanufaike na mafao ya National Social Security Fund (NSSF).
Akizungumza Februari 23, 2026 wakati wa kufungua kikao cha viongozi wa makundi maalum mkoani Mwanza, RC Mtanda amesema skimu hiyo itawasaidia wanachama wanapostaafu au wanapopoteza uwezo wa kuendelea na shughuli zao za kujipatia kipato.
Amefafanua kuwa baada ya kuchangia kwa kipindi cha miaka 15, mwanachama ataanza kupokea pensheni ya kila mwezi.
“Leo mnafanya kazi na kupata kipato, lakini miaka ijayo hamtakuwa na nguvu ileile; jiungeni sasa kujihakikishia maisha bora baadaye,” amesisitiza.
RC Mtanda ameongeza kuwa uanachama ni wa hiari kwa wote waliojiajiri na kuwa skimu hiyo inatoa kinga dhidi ya majanga kama uzee, ulemavu na ugonjwa. Amewataka viongozi kuwa mabalozi wa kuhamasisha wananchi kujiunga.
Kwa upande wake, Meneja wa NSSF Mkoa wa Mwanza Bw. Emmanuel Kihensa, amesema skimu hiyo imeanzishwa kwa mujibu wa Sheria Na. 50 ya mwaka 2018 inayoiwezesha NSSF kuwafikia waliojiajiri.
Amesema walengwa ni pamoja na wakulima, wavuvi, wafugaji, wachimbaji wadogo wa madini, mama lishe, bodaboda na wajasiriamali wengine, ambao wanapaswa kujisajili na kupatiwa namba ya malipo (control number) kwa ajili ya kuchangia.
Akizungumzia namna ya kuchangia katika skimu hiyo, Afisa Matekelezo Mkoa wa Mwanza Bw. Emmunuel Bunini amesema Mwanachama anatakiwa kuchangia angalau Sh. 30,000 kwa mwezi kwa matibabu binafsi au Sh. 52,200 kwa ajili ya matibabu yake na familia. Michango inaweza kulipwa kwa siku, wiki au mwezi kupitia benki, wakala au simu ya mkononi kwa kutumia control number.
NSSF imesisitiza kuwa lengo la skimu hiyo ni kujenga utamaduni wa kuweka akiba miongoni mwa sekta isiyo rasmi na kuhakikisha wananchi wanakuwa na uhakika wa kipato na huduma za matibabu wanapofikia umri wa kustaafu au wanapokumbwa na changamoto za kiafya.






