HATULINDWI NA DAMU YA YESU,TUNALINDWA NA MALAIKA.APOSTLE ERICK AUDAX

 

Shalom wana wa Mungu kumetokea msuguano mkubwa katika mitandao na kuleta hali ya kutokuelewana juu ya hoja ya kazi ya damu ya YESU kuwa ina nguvu ya ulinzi (Protection) huku wengine wakisema ni kwa ajili ya utakaso (Sanctification).

Hapa kuna mkanganyiko wa mapokeo na vile watu wanashindwa kutofautisha kazi ya Kristo kuja duniani.

Kristo Yesu alikuja duniani kwa ajili ya ukombozi alipigwa kwa ajili ya sisi tuwe huru kutoka katika ile laana ya torati ndio maana damu ya Yesu ina kazi ya wokovu (utakaso na ukombozi), si kwa ajili ya ulinzi, huku ulinzi ukiwa kazi ya Mungu kupitia mamlaka yake na malaika wake.

Kwanza, damu ya Yesu katika Ufunuo na nyaraka za mitume.

Ufunuo 12: 11 –12 

'Nao wakamshinda kwa damu ya Mwana-Kondoo, na kwa neno la ushuhuda wao; ambao hawakupenda maisha yao hata kufa.

 Kwa hiyo shangilieni, enyi mbingu, nanyi mkaao humo. Ole wa nchi na bahari! Kwa maana yule Ibilisi ameshuka kwenu mwenye ghadhabu nyingi, akijua ya kuwa ana wakati mchache tu.'

nao wakamshinda Shetani “kwa damu ya Mwanakondoo na kwa neno la ushuhuda wao.” Ushindi hapa si wa kimwili au wa ulinzi wa mazingira, bali ni ushindi  wa kiroho: mashtaka ya Shetani yanabatilishwa kwa sababu dhambi zimeshaondolewa. Ndiyo maana inaendelea kuzungumzia mbinguni, si mazingira ya dunia.

Ufunuo 7:14, 5:9, na 1:5 

'Nikamwambia, Bwana wangu, wajua wewe. Akaniambia, Hao ndio wanatoka katika dhiki ile iliyo kuu, nao wamefua mavazi yao, na kuyafanya meupe katika damu ya Mwana-Kondoo.'

zote zinaunganisha damu ya Yesu na kuoshwa, kutakaswa, na kununuliwa kutoka katika dhambi. Hakuna hata mstari mmoja unaosema damu inatumika kama “ulinzi” dhidi ya mashambulizi ya kazi za mwovu au ya kishetani.

Hili linaimarishwa moja kwa moja na 1 Yohana 1:7: 

 'bali tukienenda nuruni, kama yeye alivyo katika nuru, twashirikiana sisi kwa sisi, na damu yake Yesu, Mwana wake, yatusafisha dhambi yote.'

damu ya Yesu “hututakasa dhambi zote.”

Vivile, 1 Petro 1:18–19 

'Nanyi mfahamu kwamba mlikombolewa si kwa vitu viharibikavyo, kwa fedha au dhahabu; mpate kutoka katika mwenendo wenu usiofaa mlioupokea kwa baba zenu;

 bali kwa damu ya thamani, kama ya mwana-kondoo asiye na ila, asiye na waa, yaani, ya Kristo.'

inaeleza kuwa tulinunuliwa kwa damu ya thamani ya Kristo, si kwa fedha au dhahabu au vitu viharibikavyo. Hapa lugha ni ya ukombozi (redemption), si ya ulinzi (protection).

Kwa hiyo, kazi ya Mwanakondoo kulingana na Agano Jipya ni mbili kuu:

– Kutusafisha dhambi (expiation / cleansing)

– Kutununua kutoka utumwani mwa dhambi na mauti (redemption).

Waebrania 9:22 

Na katika Torati karibu vitu vyote husafishwa kwa damu, na pasipo kumwaga damu hakuna ondoleo.

Hii inaweka damu ndani ya mfumo wa haki ya Mungu, si ndani ya mfumo wa vita vya kiroho.

Pili, ulinzi ni kazi ya Mungu kupitia malaika, si damu ya Yesu.

Zaburi 34:7

 'Malaika wa Bwana hufanya kituo, Akiwazungukia wamchao na kuwaokoa.'

Inasema malaika wa Bwana hufanya kuzunguka wamchao Bwana na kuwaokoa.

Waebrania 1:4–5, 7 

'amefanyika bora kupita malaika, kwa kadiri jina alilolirithi lilivyo tukufu kuliko lao.'

inaeleza kuwa malaika ni roho zitumikazo, waliotumwa kuwahudumia wale watakaourithi wokovu.

Waebrania 12:22

'Bali ninyi mmeufikilia mlima Sayuni, na mji wa Mungu aliye hai, Yerusalemu wa mbinguni, na majeshi ya malaika elfu nyingi'

 inaonyesha wazi kuwa watu wanaomwambudu Bwana wamefika “mlima Sayuni… na mkutano wa malaika elfu nyingi.’’

Ufunuo 12:7 inaonyesha wazi kuwa vita dhidi ya Shetani mbinguni vinapiganwa na Mikaeli na malaika zake, si damu. Damu tayari ilikuwa imetimiza kazi yake ya Kiungu; vita vya utekelezaji vinafanywa na malaika kwa mamlaka ya Mungu.

Mathayo 13:49 

 'Ndivyo itakavyokuwa katika mwisho wa dunia; malaika watatokea, watawatenga waovu mbali na wenye haki'

na Luka 16:22 

'Ikawa yule maskini alikufa, akachukuliwa na malaika mpaka kifuani kwa Ibrahimu. Yule tajiri naye akafa, akazikwa.'

zinaonyesha tena kazi ya malaika katika kutenganisha, kubeba, na kulinda mipaka ya haki ya Mungu.

Tatu, Yesu mwenyewe hakutumia “damu” kama hoja ya ulinzi.

Mathayo 4:6 

 'Akamwambia, Ukiwa ndiwe Mwana wa Mungu jitupe chini; kwa maana imeandikwa, Atakuagizia malaika zake; Na mikononi mwao watakuchukua; Usije ukajikwaa mguu wako katika jiwe.'

Shetani anapomjaribu Yesu kwa Zaburi 91, Yesu hakujibu kwa “nitajifunika kwa damu,” bali kwa Neno la Mungu lililoandikwa.

Mathayo 26:47–54 

  Basi alipokuwa katika kusema, tazama, Yuda, mmoja wa wale Thenashara akaja, na pamoja naye kundi kubwa wenye panga na marungu, wametoka kwa wakuu wa makuhani na wazee wa watu.

 Na yule mwenye kumsaliti alikuwa amewapa ishara, akisema, Nitakayembusu, huyo ndiye; mkamateni.

 Mara akamwendea Yesu, akasema, Salamu, Rabi, akambusu.

 Yesu akamwambia, Rafiki, fanya ulilolijia. Wakaenda, wakanyosha mikono yao wakamkamata Yesu.

 Na tazama, mmoja wao waliokuwa pamoja na Yesu akanyosha mkono wake, akaufuta upanga wake, akampiga mtumwa wa Kuhani Mkuu, akamkata sikio.

 Ndipo Yesu akamwambia, Rudisha upanga wako mahali pake, maana wote waushikao upanga, wataangamia kwa upanga.

 Ama wadhani ya kuwa mimi siwezi kumsihi Baba yangu, naye ataniletea sasa hivi zaidi ya majeshi kumi na mawili ya malaika?

 Yatatimizwaje basi maandiko, ya kwamba hivyo ndivyo vilivyopasa kujiri?

Yesu anakataa kutumia nguvu au ulinzi wa malaika, ingawa anasema angeweza kuomba malaika zaidi ya kumi na mbili elfu. Hii inaonyesha kuwa ulinzi unatolewa kwa mamlaka ya Mungu Baba.

Kwa hivyo kwa lugha ya kitaalamu damu ya Kristo inafanya kazi katika soteriology (wokovu), si katika angelology ya utekelezaji wa ulinzi.

Ninlazima kuelewa kuwa Damu ya Yesu ina nguvu sana katika kuleta wokovu , utakaso, na ushindi wa Kiungu dhidi ya dhambi na hukumu ya Shetani.

Lakini ulinzi unatoka kwa Mungu kupitia mamlaka yake, pamoja na Neno lake, na malaika Wake.

Kutumia damu yake Yesu kama sehemu ya kujikinga au kujilinda hii ni kutoka nje ya neno la Mungu na kutumia hisia pamoja na akili zako mwenyewe.

Umebarikiwa.Apostle Erick Audax



Post a Comment (0)
Previous Post Next Post