MME NA MKEWE WAFARIKI DUNIANI JIJINI MWANZA,CHANZO UGOMVI WA KIFAMILIA

 

Jeshi la polisi mkoa wa Mwanza limetoa taarifa ya matukio ya vifo vya watu wawili ambao ni mtu na mke wake vilivyotokea tarehe 28.09.2024 na 30.09.2024 katika wilaya ya Ilemela na Nyamagana.

 Ni kwamba, mnamo tarehe 28.09.2024 majira ya 22.45hrs katika mtaa wa Nyamhongolo, wilaya ya Ilemela, mwanamke aitwae Rausa Mohamed, miaka 36, mfanyabiashara na mkazi Nyamhongolo alisukumwa na kuanguka kwenye sakafu kisha kujeruhiwa kwa kuchomwa na kitu chenye ncha kali shingoni na mume wake aitwae Dervinus Nkabatina, miaka 46, mfanyabiashara na mkazi wa Nyamhongolo baada ya kuzuka ugomvi uliotokana na mgogoro wa kifamilia. 


Baada ya tukio hilo majirani walifika kwa ajili ya kutoa msaada na taarifa zilifika kwa Jeshi la polisi, hatimae mgonjwa alipelekwa katika kituo cha afya Igoma. Wakati madaktari wanajaribu kuokoa maisha yake alifariki dunia. Mtuhumiwa baada ya tukio hilo alikimbia kusiko julikana na jitihada za kumtafuta zilianza mara moja. Marehemu Rausa Mohamed ameacha mtoto mwenye umri wa mwaka mmoja.

Jeshi la polisi likiwa linaendelea na msako wa kumtafuta mtuhumiwa Dervinus Nkabatina kwa kushirikiana na wananchi lilitoa taarifa sehemu mbalimbali ili Mtuhumiwa akionekana aweze kukamatwa.Ilipofika tarehe 30.09.2024 majira ya 13.00hrs zilipatikana taarifa kuwa mtuhumiwa Dervinus Nkabatina ameonekana akiwa anakunywa pombe katika bar ijulikanayo kwa jina la Ndama.


 Jeshi la Polisi lilifika katika bar hiyo na kumkuta mtuhumiwa akiwa amedhoofika. Jeshi la polisi lilipata taarifa kutoka kwa wahudumu wa bar hiyo kuwa mtuhumiwa Dervinus Nkabatina alifika katika bar hiyo akiwa ameshika bahasha yenye rangi ya khaki na kuagiza pombe aina ya konyagi chupa yenye ujazo wa miligram 750, kisha alimeza vidonge ambavyo idadi yake haikuweza kufahamika kwa kutumia pombe aliyokuwa ameagiza ndipo hali yake ilianza kubadilika ikawalazimu watoe taarifa kwa Jeshi la polisi. 


Askari wa Jeshi la polisi walifika na kumfanyia upekuzi katika maungo yake na kukuta mabaki ya dawa aina ya Metronidazole na kiasi cha pombe aina ya konyagi kwenye chupa, pia alikutwa na karatasi yenye ujumbe usemao “Shetani ameanza kuniita ewe Mwenyezimungu roho yangu naikabidhi mikononi mwako”. Karatasi hiyo pia ilikuwa na maandishi mengine yanayoonesha majuto ya kitendo cha kumuua mke wake na kuwa amefanya maamuzi ya kujiua na angependa mwili wake usipelekwe kwao Karagwe bali uzikwe Mwanza. Dervinus Nkabatina alikimbizwa katika hospital ya Sekeo-Toure hata hivyo alifariki dunia wakati matibabu yakiendelea.

Chanzo cha matukio haya ni wivu wa kimapenzi, kwani inadaiwa mwanamke alikuwa akimtuhumu mume wake kuwa na mahusiano ya kimapenzi na wanawake wengine na mume wake aliamua kujiua ili kukwepa mkono wa sheria baada ya kufanya maamuzi yasiyo faa kwa kumshambulia mke wake na hatimae kumuua.


 Jeshi la polisi mkoa wa Mwanza linatoa wito kwa wananchi kuacha kujichukulia sheria mkononi na badala yake kutumia njia sahihi ya kutatua changamoto zao kwa kushirikisha viongozi wa dini, wazazi, wadau mbalimbali wanaohusika kutoa ushauri nasaha ili kuzuia matukio kama haya. Pia, waendelee kutoa taarifa za uhalifu na wahalifu ili ziweze kufanyiwa kazi kwa haraka. 

Aidha, Jeshi la polisi linapenda kutoa taarifa kuwa tarehe 01.10.2024 limewafikisha mahakamani watuhumiwa, Robart Kabota na wenzake watatu ambao walihusika katika suala la mtumbwi uliozama kule wilaya ya Ilemela,watuhumiwa hao wamefikishwa mahakamani na kusomewa makosa yao baada ya maelekezo kutoka ofisi ya mkuu wa Mashtaka kwamba washtakiwe. Mtakumbuka kwamba jalada hilo lilipelekwa katika ofisi ya mkuu wa mashtaka kwa ajili ya mwongozo wa kisheria na sasa maamuzi yametoka na wameweza kushtakiwa katika mahakama ya wilaya ya Ilemela na kusomewa shtaka namba 28049/2024 la kosa la kuua bila kukusudia, watuhumiwa wamepelekwa gereza la Butimba hadi tarehe 15.10.2024.


 Aidha, tunaendelea kuwakumbusha wananchi wote kuendelea kuzingatia maelekezo yote yanayotolewa na Serikali ya kupanda vyombo vya usafiri majini ambavyo vimesajiliwa rasmi kwa taratibu zilizowekwa na mamlaka husika. Pia, tunawakumbusha watoa huduma za usafirishaji katika ziwa victoria kufanya kazi kulingana na leseni zao, kwa sabababu kutofanya hivyo ni uvunjifu wa sheria na kuhatarisha usalama wa watu na mali zao. 

Na Pascal Kadushi

Post a Comment (0)
Previous Post Next Post