MRADI WA RUMAKALI (222MW) SASA UNAANZA KUTEKELEZWA - DKT. BITEKO

 

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko amesema kuwa, mradi wa umeme wa maji wa  Rumakali utakaozalisha megawati 222 uliopo wilayani Makete mkoani Njombe sasa unaanza kutekelezwa ikiwa ni utekelezaji wa maagizo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuwa, vyanzo vyote vya umeme sasa viendelezwe.

Dkt. Biteko amesema hayo tarehe 22 Februari 2024 wilayani Makete mkoani Njombe mara baada ya kutembelea eneo lenye maporomoko ya maji ya Mto Rumakali ambapo tuta la kuzuia maji yatakayozalisha umeme litajengwa pamoja na mitambo ya kuzalisha umeme

“Upembuzi yakinifu wa mradi huu ulifanyika kwa mara ya kwanza mwaka 1998 na uhuishaji wake ukafanyika mwaka 2022 ambao ulionesha kuwa mradi unatekelezeka na una manufaa ya kiuchumi na kijamii hivyo maagizo ya Dkt. Samia Suluhu Hassan ni kuanza kuutekeleza ili kuongeza vyanzo vya umeme.” Amesema Dkt. Biteko


Amesema kuwa, pamoja na utekelezaji wa mradi wa umeme Julius Nyerere (JNHPP) utakaozalisha megawati 2115 lakini maendeleo makubwa yanayoendelea kutokea katika nchi yatahitaji umeme mwingi na hivyo Serikali inapata msukumo wa kuendeleza vyanzo vingine vya umeme ikiwemo mradi huo wa Rumakali.

Ameeleza kuwa, hatua inayofuata kwenye mradi huo ni utafutaji wa mjenzi ambaye atapatikana kwa njia ya ushindani wa tenda.

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko

 


Imeandaliwa na Pascal Kadusi

Post a Comment (0)
Previous Post Next Post