Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Tabora, Hassan Wakasuvi amefariki dunia ghafla akiwa ofisini kwake mkoani humo.
Katibu Mwenezi wa CCM Mkoa wa Tabora, Iddy Mambo amethibitisha kifo cha kiongozi huyo wa chama na kusema mwili wake umehifadhiwa katika Hospitali ya Rufaa ya Kitete mkoani humo.
Mambo amesema mwenyekiti huyo amefariki akiwa ofisini kwake wakati akisuburia ugeni wa Mwenyekiti wa Jumuiya Wazazi CCM Taifa, Fadhil Maganya, aliyetarajiwa kuanza ziara yake ya chama mkoani humo.
“Ni kweli kabisa Mzee wetu, Mwenyekiti wa CCM mkoa wa Tabora na mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM ametutoka, muda kama saa 8:30 mchana, ameamka leo akawa anadai kwamba hajisikii vizuri, lakini akaja ofisini kwa maana tulikuwa na shughuli ya kumpokea mwenyekiti wa wazee Taifa ambaye alikuwa na ziara ya siku nne katika mkoa wetu.
“Wakati tunasubiria pale basi akasema alikuwa ana changamoto anasikia jasho linamtoka kwa wingi na hajisikii, kwa hiyo akabaki ofisini kwa ajili ya kutusubiria. Sisi tulivyokwenda kumpokea mwenyekiti wa wazazi Taifa, nikapigiwa simu kwamba mzee wetu anaumwa kwa hiyo nilivyoenda kumchukua kwa ajili ya kumpeleka hospitalini tukiwa njiani bahati mbaya kumbe alikuwa ameaga dunia,” amesema Mambo.
Mwenezi huyo amesema Wakasuvi ambaye alikuwa mwenyekiti wa CCM mkoa mwenye umri mkubwa, atakumbukwa kwa uzalendo ndani ya chama, uwezo wa kusimamia na kutopenda uonevu jambo linalotajwa kumfanya adumu kwenye siasa za chama hicho.
Naye, Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Tabora ya Kitete, Mark Waziri, amekiri kumpokea mwenyekiti huyo na kusema baada ya vipimo kufanyika ilibainika alikuwa ameshafariki kabla ya kufikishwa hospitalini hapo.

.jpg)