Miaka miwili iliyopita, Tinasoa Rakotoarimanana mwenye umri wa miaka 24 hakushtuka alipoanza kuona mabaka mekundu usoni mwake na mikononi.
Lakini mara akaanza kuhisi ganzi kwenye vidole vyake hivyo akaamua kwenda katika kituo cha afya katika kitongoji cha Miarinarivo katikati mwa Madagasca. Na majibu aliyoyapata, ndiyo yaliyoibua hofu ya maisha.
‘’Nililia. Nilihisi kama maisha yangu yamesimama,’’ Tinasoa aliiambia TRT Afrika. ‘’Niliogopa kwamba hakuna mtu angenitaka tena, hasa kwa sababu mimi ni kijana,’’ anaongeza.
Na ukweli kwa hofu yake ulidhihirika. Taarifa za ugonjwa wake zilianza kuenea kijijini, na pole pole watu wakaanza kumtenga. Idadi ya marafiki aliokuwa nao ikapungua, na wengine wakawa hawana muda tena na yeye. Kila mmoja aliogopa kuambukizwa.
‘’Katika kijiji changu, baadhi ya watu walisema ugonjwa wa ukoma ulitoka kwa familia yangu, na wengine walisema ni laana. Lakini hakuna mtu katika historia ya familia yangu aliyewahi kuugua ukoma,” anasema.
Lakini upande wa pili wa mji, Solo Andrianirina mwenye umri wa miaka 32, nae alikuwa na tatizo kama hilo.
Anakumbuka, kwa mara ya kwanza alipoambiwa kuwa ameambukizwa ukoma.‘’Niliogopa. Kwangu mimi, ukoma ulikuwa ugonjwa wa zamani, jambo baya sana. Mara moja nilifikiria kutengwa na aibu,’’
WHO inasema ugonjwa wa ukoma unasalia kuwa tatizo kubwa la afya ya umma, ingawa maendeleo yamepatikana katika miongo kadhaa iliyopita.
Kulingana na takwimu za hivi karibuni, Mwaka 2023, maambukizi mapya 21,043 ya ukoma yaligunduliwa katika Kanda ya Afrika, ikiwa ni asilimia 11.5 ya jumla ya dunia.
Nchi nyingi zimefanikisha kutokomeza rasmi ukoma kama tatizo la afya ya umma - uliowekwa katika kiwango cha chini cha maambukizi 1 kwa kila watu 10,000 - lakini mifuko ya maambukizi ya juu zaidi imesalia, hasa katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Ethiopia, Madagasca, Msumbiji, Nigeria, na Tanzania.
Wataalamu wanasisitiza kuwa ingawa viwango vya maambukizi na ugunduzi vinapungua, maambukizi bado yapo, utambuzi wa kuchelewa, na ulemavu unaohusishwa bado unatokea.
Mnamo 2023, jumla ya maambukizi 3,000 ya Ukoma kiwango cha Daraja la 2 - alama ya kuchelewa kugunduliwa - yaliripotiwa barani Afrika.
Tatizo la Ukoma ni kuwa kadri inavyozidi kutokomezwa ndivyo waathirika wanavyozidi kunyanyapaliwa kwa kuonekana wanaugua maradhi ya kale.
Ingawa ukoma ni nadra, bado unaambukiza na hupitishwa kwa njia ya hewa, si kwa kugusa.
Hii inamaanisha kuwa bakteria hupitishwa kupitia matone madogo kutoka kwa pua na mdomo wakati mtu aliyeambukizwa anakohoa au kupiga chafya. Mgusano wa kawaida kama vile kupeana mikono, kukumbatiana, kushiriki chakula, kukaa karibu na mtu, hakuenezi ukoma. Zaidi ya 95% ya watu wana kinga ya asili.
WHO inasema uambukizaji wa Ukoma ni chini hata kuliko magonjwa kama vile TB, COVID-19, au surua na mgonjwa anapoanza matibabu, uwezo wake wa kuambukiza hufifia haraka sana.
Hata hivyo hofu yao ya unyanyapaa inazuia watu wengi kujitokeza kwa ajili ya matibabu, na kusababisha matatizo ya muda mrefu na maambukizi ya ukoma yanayoendelea.


.webp)