Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, ametenga shilingi bilioni tano kwa ajili ya kuwawezesha wasanii nchini kote kupitia mfuko maalum wa utamaduni na sanaa. Lengo la hatua hiyo ni kuinua sekta ya sanaa kwa kuwapa wasanii mitaji itakayowawezesha kupanua kazi zao, kujiajiri na kuongeza kipato chao. Mpango huo unatajwa kuwa fursa muhimu kwa vijana na wadau wa tasnia ya ubunifu nchini.
Katika kutekeleza mpango huo, Mfuko wa Utamaduni na Sanaa umefika jijini Mwanza kutoa semina maalum kwa wasanii wa mkoa huo. Semina hiyo imelenga kutoa elimu kuhusu namna ya kuomba na kunufaika na mkopo huo, pamoja na kuwajengea uwezo wa kusimamia fedha watakazopatiwa ili ziweze kuleta tija katika shughuli zao za kisanii.
Akizungumza wakati wa semina hiyo, mmoja wa waratibu, Jovita Godwin, alieleza kuwa upatikanaji wa fedha hizo utafanyika kupitia benki kwa utaratibu maalum uliowekwa. Alisisitiza kuwa lengo la mpango huo si kuwakandamiza wasanii, bali kuwawezesha kuchukua mikopo na kuirejesha kwa wakati ili mfuko uweze kuwahudumia wasanii wengi zaidi nchini.




