Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe. Said Mtanda ameutangazia umma kuhusu mapokezi ya mbio za mwenge Mkoani humo unaotarajiwiwa kupokelewa oktoba 06, 2024 katika Kijiji cha Nyamadoke kilichopo Halmashauri ya Wilaya ya Buchosa ukitokea Mkoa wa Geita.
Mhe. Mtanda ametoa Taarifa hiyo mapema leo oktoba 01, 2024 ofisini kwake alipokuwa akizungumza na Waandishi wa Habari, Mkuu huyo wa Mkoa amesema Mwenge wa Uhuru utakimbizwa katika Halmashauri 8 kwa umbali wa kilometa 627.
Aidha RC Mtanda amesema Mwenge wa uhuru 2024 ukiwa Mkoani Mwanza utafikia jumla ya miradi ya maendeleo 58 inayogharimu kiasi cha Tsh. Bilioni 99,370,447,286.76 ambapo kati ya hizo wananchi wa Mkoa wa Mwanza wamechangia milioni 2,615,713 576.00.
"Kati ya fedha hizo Halmashauri zimechangia milioni 2,775,384,864.08 huku Serikali Kuu bilioni 19,704,775,674.99 na washirika wa maendeleo bilioni 74,274,573,171.69". Amesema Mhe. Mtanda.
Mhe. Mtanda ameendelea kwa kusema Mkoa wa Mwanza umepewa heshima ya kuwa mwenyeji wa Maadhimisho ya kilele cha Mbio za Mwenge wa uhuru Kitaifa 2024, Wiki ya Vijana na Miaka 25 ya Kumbukizi ya Kifo cha Baba wa Taifa Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere 199-2024.
Na Erick Audax


