Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan amekipongeza Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo kufanikisha katika mchakato wa uandishi wa kitabu cha aliyewahi kuwa Waziri Mkuu wa Tanzania, Hayati Edward Moringe Sokoine.
Rais Samia ametoa pongezi hizo wakati akishiriki uzinduzi wa kitabu cha Uongozi na Maisha ya Hayati Sokoine Jijini Dar Es salaam kilichozinduliwa katika ukumbi wa mikutano wa JNICC. Amesema kuwa SUA kimekuwa Chuo kinachoishi maono ya Hayati Sokoine mpaka sasa na kufanya historia yake iendelee kuishi kwa kupitia Chuo hicho
Aidha, Mhe. Rais amewataka vijana hususani viongozi vijana kuwa wachapakazi kama alivyokuwa Hayati Sokoine na hata kuaminiwa akiwa na umri mdogo na kupewa madaraka makubwa ya kuwa Waziri Mkuu wa Tanzania. Pia amewaomba Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora kuwawezesha viongozi walio hai waweze kuandika historia zao katika vitabu .
Kwa upande wake Mkuu wa Chuo hicho Mhe. Jaji Joseph Sinde Warioba amemuelezea Hayati Sokoine kama kiongozi shujaa na aliyeweza kuishi maisha ya kimaskini, lakini pia akisimamia sheria kwa ajili ya kupambana na wabadhilifu na wala rushwa nchini, huku akitoa mifano yake mbalimbali wakati wa uhai wake.
Naye Makamu Mkuu wa Chuo cha SUA Prof. Raphael Chibunda ameelezea chimbuko la Chuo cha Sokoine cha Kilimo huku akiweka wazi uhusiano uliopo kati ya Waziri Mkuu huyo na Chuo hicho huku akieleza namna maamuzi ya kuanzishwa kwa Chuo hicho yalivyotolewa na Waziri Mkuu huyo Aprili 11 mwaka 1984 katika Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Prof. Chibunda ameongeza kuwa Chuo kikuu cha Sokoine cha Kilimo kimekuwa kikimuenzi Hayati Sokoine kila mwaka kuanzia mwaka 1992 kwa kuanzishwa kwa mhadhara wa kumuenzi.
Na mwandishi wetu-Dar


