Taasisi ya uhasibu Kampasi ya Mwanza inatarajia kuokoa fedha kiasi cha zaidi ya Shilingi milioni mia tano zilizokuwa zikitumika kulipia kodi ya pango baada ya Serikali kukamilisha ujenzi wa mradi wa chuo cha taasisi hiyo kilichopo eneo la Nyangh’omang’o Wilayani Misungwi Mkoani Mwanza.
Akikabidhiwa jengo hilo la chuo kutoka kwa wakandarasi waliopewa zabuni ya ujenzi huo CRJE , Afisa Mtendaji Mkuu wa Taasisi hiyo Prof. William Pallangyo amesema mradi huo wa chuo cha TIA mkoani Mwanza umegharimu kiasi cha shilingi Bilioni 7.8 na kwamba mradi huo pia umeleta fursa ya ajira kwa wakazi zaidi ya 1500 wa maeneo hayo.
“Tunaishukuru sana Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Mhe. Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kwa ujenzi wa chuo hiki ambacho kitaenda kusaidia vijana watakaochaguliwa kujiunga na kuanza masomo kwa mwaka wa masomo ambao unaanza mwezi wa kumi mwaka huu” .Amesema Prof. Pallangyo
Prof Pallangyo ameongeza kuwa chuo hicho kinatarajia kupokea zaidi ya wanafunzi 2000 kutoka katika maeneo mbalimbali nchini na kuwataka wanafunzi watakaotumia majengo ya chuo hicho kuyatunza ili yaweze kudumu kwa muda mrefu.
Kwa upande wake Mkandarasi mshauri wa mradu huo Dkt. Mihanda Manyahi amesema kuwa ujenzi wa mradi huo ulianza mwaka 2022 ambapo hadi sasa (July 2024) wamekamilisha ujenzi huo na kuukabidhi licha ya kuwepo kwa changamoto za kijografia ya eneo hilo kuwa na miamba wakati wa kuandaa eneo la mradi hali iliyopelekea kuongeza muda wa ukamilishaji wa mradi.
“Tunaishukuru serikali kwa kutuamini na kutukabidhi mradi huu ambao tumeutekeleza na leo hii tumeukabidhi ndani ya wakati ukiwa na jumla ya majengo makubwa matatu ya ghorofa, ”amesema Dkt. Manyahi.
Nae Mkurugenzi wa Kampasi ya TIA Mwanza Dkt. Honest Kimario amesema Chuo hicho kina miundombinu ya kisasa inayojumuisha huduma za kijamii ikiwemo maji, umeme pamoja na barabara ambazo tayari zimewekwa katika eneo hilo la chuo na kwamba wanatarajia kupata wanafunzi wa kimataifa kutoka nje ya nchi.
Na Pascal Kadushi



