Waziri wa Madini Mhe. Anthony Mavunde (MB), akiwa ameambatana na Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe. Rosemary Senyamule wamefanya ziara kwenye Kijiji cha Mwinyi kilichopo katika Kata ya Handali, Wilaya ya Chamwino kufuatia mgogoro ulioibuka kwenye eneo hilo maarufu kwa uchimbaji mdogo wa Madini.
Mgogoro huo kati ya mwekezaji na wachimbaji hao, umetajwa kuanza mapema mwaka huu kwa mwekezaji kuzuia wachimbaji hao kuendelea na shughuli zao za kawaida kwa kuleta wageni katika eneo hilo hali iliyosababisha sintofahamu.
Baada ya kusikiliza upande wa walalamikaji (wachimbaji wadogo), Mhe. Mavunde ametoa maagizo kadhaa kwa wachimbaji hao na mwekezaji mzawa ambaye anajulikana kwa jina la Juma Nkamia.
"Hatuwezi kufanya Watanzania watumwa ndani ya nchi yao kwani wanatumia nguvu zao hapa. Sheria ya madini inasema, mwenye leseni hataendelea na shughuli zake mpaka haki ya mwenye ardhi hivyo Mmiliki akubaliane na mwekezaji wakubaliane juu ya wachimbaji wenye maduara.
"Kuanzia Sasa, asiingie mgeni yeyote eneo hili mpaka Suluhu itakapopatikana. Natoa muda hadi siku ya Jumatano, Julai 10, Mwekezaji na kiongozi wa wachimbaji wa eneo hili, mufike ofisini kwangu, tuongee na kulimaliza suala hili ili kila mmoja aweze kuendelea na shughuli zake" Ameagiza Mhe. Mavunde
Naye Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe. Rosemary Senyamule ambaye ndiye Mwenyekiti wa Kamati ya usalama ya Mkoa, amewataka wakazi wa eneo hilo kutumia fursa ya upatikanaji wa Madini kama Baraka.
"Mkoa unatarajia Baraka ya Madini itumike kuwanufaisha wanadodoma. Kazi yetu kubwa ni kuhakikisha Amani na usalama kwa wananchi wote wa Mkoa wa Dodoma. Polisi waingie kazini kuchunguza jambo hili ili haki itendeke na Mkoa tutaendelea kufuatilia kila kinachoendelea hapa. Amesema Mhe. Senyamule.
Eneo hilo linalosadikika kuwa na madini, lilianzishwa rasmi mwaka 2020 na kina mama walikua wakifagia eneo hilo lakini hadi kufikia Februari 2024, zilisikika fununu za kuuzwa kwa mwekezaji. Tangu kupatikana kwa mwekezaji huyo, ndipo mgogoro ulipoibuka kutokana na mwekezaji huyo kutoa taarifa kwamba wachimbaji hao wasimamishe shughuli zao na kuhama eneo hilo.





