FAMILIA zimetakiwa kutoa elimu ya hedhi salama kwa watoto wa kike ili waweze kuona suala la hedhi ni jambo la kawaida.
Rai hiyo imetolewa leo na Naibu Katibu mkuu wa Wizara ya Afya, Dkt. Grace Magembe wakati wa kongamano la Kitaifa la wadau wa Sekta ya Afya kuhusu maandalizi ya Dira ya Taifa ya maendeleo 2050 iliyofanyika katika ukumbi wa mikutano wa kimataifa wa Mwalimu Nyerere(JNICC).
‘’ Familia zisaidie watoto wa kike kwa ujumla katika utoaji wa elimu ya hedhi salama ili kujiandaa kisaikolojia na watoto wa kike waweze kuona hedhi ni kitu cha kawaida katika makuzi yao’’ amesema.
Amezishauri familia zione suala la Hedhi salama ni sehemu ya maisha ya mtoto wa kike. Dkt.Magembe amesema Kampeni ya Mtu Ni Afya, inaendana sambamba na uandaaji wa dira ya maendeleo 2050 kwakuwa kampeni hiyo inachangia katika uandaji wa dira ya maendeleo 2050.
‘’Ili tuweze kuwa na maendeleo yoyote, lazima tuwe na Afya bora huwezi kuwa mtu umekamilika kama wewe ni mgonjwa’’ amesema.
Akielezea zaidi kuhusu kampeni ya Mtu Ni Afya, Dkt. Magembe amesema kampeni inaongelea usafi wa mazibgira ikiwemo na matumizi ya vyoo safi pamoja na matumizi ya maji safi na salama.
Katika hatua nyingine, Ameitaka jamii kuepeuka matumizi ya vilevi kama pombe pamoja na kuepuka kutumia chumvi nyingi iliyopitiliza.
Ameshauri pia jamii iwe na mtindo bora wa maisha ni lazima kufanya mazoezi ya mwili ili mwili uwe salama.
Naye Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu amesema mipango ya Serikali ni kuwa kila mtanzania ifikapo 2050 ni lazima awe na Afya bora.
‘’ Kwenye sekta ya Afya, tunaguswa sana na masuala lishe. Pia kama Sekta ya Afya jukumu letu ni kuhakikisha upatikanaji wa Afya bora kwa watu wote na kuzingatia upatikanaji wa maji safi na salama’’ amesema.
Waziri Ummy ameitaka jamii kuwa na utaratibu wa kufanya mazoezi na kuzingatia ulaji mzuri wa chakula.
Amesema licha ya juhudi mbalimbali zilizofanywa na Serikali katika kuboresha sekta ya Afya bado kuna tatizo kubwa sana la magonjwa yasioambukizwa ikiwemo shinikizo la damu,Kisukari na Afya ya Akili.
‘’ Tumefanya vizuri sana kama Sekta ya Afya katika miaka 25 iliyopita ila bado ipo kazi kubwa sana tunatakiwa tufanye ili tuweze kufikia lengo la Afya bora kwa wote’’ amesema.


.jpeg)
