"Wazazi na walezi zungumzeni watoto wenu ili mjue madhila wanayo pitia aidha majumbani, mitaani na shuleni. Pia mzazi ni lazima ujue tabia ya mwanao na endapo umegundua mtoto amefanyiwa ukatili au ubakaji toa taarifa usikae kimya"
Hayo yamesemwa Machi 24, 2024 na kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma Kamishna msaidizi mwandamizi wa Polisi Theopista Mallya wakati akizungumza na waumini wa kanisa katoliki la Mt. Paul wa Msalaba jimbo kuu Dodoma.
Kamanda Mallya amesema kumekuwa na kesi ambazo zimekuwa zikiripotiwa za matukio ya ubakaji na ulawiti kwa watoto lakini jamii haichukui hatua ili kudhibiti matukio hayo kwa jamii na kuamua kusuluhisha majumbani jambo ambali ni kinyume na sheria.
"Wazazi msisuluhishe kesi kienyeji na kujuana, kufanya hivyo nikuendekeza matukio haya na ni ukatili kwa wahanga, simamieni ipasavyo toeni taarifa kwa Jeshi la Polisi ni kutoa ushahidi mahakamani mpaka mwisho." amesema Kamanda Mallya.
Katika hatua nyengine Mallya amekemea vitendo vya ukatili vinavyo sababishwa na wivu wa kimapenzi na kusababisha matukio ya mauaji kwa jamii. Huku paroko wa parokia Mt. Paul Michael Gaula akiwataka waumini wakanisa hilo kutafakari mienendo walio nayo nakumrudia mwenyezi Mungu na kutenda yalio mema.
Aidha kamanda Mallya ameendelea na ziara katika nyumba za ibada na mikusanyiko ya watu kwa lengo la kutoa elimu ya ulinzi na usalama pamoja na kuongea na wakazi wa Dodoma.
By Pascal Kadusjhi
