Mkuu wa Jeshi la Polisi Nchini IGP Camilius Wambura ameguswa na kitendo cha waendesha pikipiki wa Gairo (bodaboda) kuikubali dhana ya Polisi Jamii na kuamua kushirikiana na Jeshi la Polisi katika kuzuia uhalifu.
Ikumbukwe Machi 13, 2024 Bodaboda wa Gairo walitamba kwenye mtandao wa Instagra ya Polisi baada ya kukusanyana na kwenda kituo cha Polisi Gairo kuwapongeza Askari kwa utendaji wao hususani kwa kuwafikia kwenye vijiwe vyao na kuwapa elimu. Na siku inayofuata bodaboda hao walirudi tena kituoni hapo na kusaidia kwa pamoja kuchimba Msingi wa ujenzi wa ofisi za Dawati la Jinsia na watoto pamoja na Polisi Jamii.
Akiwasilisha salamu hizo za pongezi machi 23, 2024 Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi ( SACP) Alex Mkama amesema, wamekuwa wakiihubiri Polisi Jamii kwa muda mrefu katika maeneo yote ya Mkoa wa Morogoro ila Bodaboda wa Gairo wamekuwa wa kwanza kuikubali kwa vitendo jambo ambalo litapunguza uhalifu katika maeneo hayo.
Naye Mkuu wa Polisi Jamii Wilaya hiyo hakusita kutoa pongezi kwa bodaboda hao kwa ushirikiano na kuwataka wawe mabalozi wazuri wa kuyatangaza mazuri ya Jeshi la Polisi kwenye maeneo yao.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Bodaboda hao amesema kuwa, wamefanya hivyo baada ya kuona wameheshimiwa na kuthaminiwa sana na Jeshi la Polisi kwa kitendo cha kuwafuata kwenye vijiwe vyao na kuwapa elimu na sio kuviziana na kukamatana kama ilivyo hapo zamani.
