Katika kuhamasisha ulinzi shirikishi, Afisa Polisi Jamii Mkoa wa Mwanza kamishna msaidizi wa Polisi (ACP) Ramadhani Sarige amegawa mipira miwili kwa timu za soko la Kimataifa la dagaa la Mwaloni na soko la matunda na mbogamboga Magomeni yalilopo Kata ya Kirumba mkoani humo.
Akizungumza na wafanyabiashara hao, ACP Sarige amesema Jeshi la Polisi limetoa mipira hiyo kwa wachezaji wa timu hizo ili kuwawezesha kujifua kuelekea mchezo wa soka kati ya timu ya soko la dagaa na soko la mbogamboga na matunda, utakaopigwa Aprili 21, mwaka huu
"Kwa niaba ya Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza tumetoa mipira hii kwa timu zote mbili za masoko haya ili kujiandaa na mechi ambayo itachezwa tarehe 21 April 2024 katika uwanja wa Furahisha Kirumba lengo kuu likiwa ni kushirikiana na jamii katika kupeana elimu ya ulinzi shirikishi ili kuzuia uhalifu,” amesema ACP Sarige.katika uwanja wa Furahisha mkoani humo.
Kwa upenda wake, Mwenyekiti wa soko la mbogamboga na matunda Magomeni, Ramadhani Maganga Nsululu amelipongeza Jeshi hilo kwa jitihada zake za kuzuia uhalifu kupitia dhana ya ulinzi shirikishi ambapo amesema ushirikiano huo utasaidia kutokomeza uhalifu mkoani humo.
"Tunalishukuru Jeshi la Polisi kwa kutuletea mipira hii itasaidia vijana kujiandaa kwa mechi hiyo lakini pia juhudi za Jeshi kutoa elimu ya ulinzi zimesaidia wananchi kutoa taarifa za uhalifu na kuishi kwa amani,” amesema Nsululu.
Awali wiki iliopita.
ACP Sarige alipotembelea eneo hilo aliahidi kutoa mipira ya soka kwa timu za wafanyabiashara hao ahadi ambayo ameitimiza ndani ya wiki moja ili kujenga mahusiano kati yao, mahusiano hayo yatasaidia kujenga ushirikiano wa kutokomeza uhalifu na kuhamasisha ulinzi shirikishi kwa jamii mkoani humo.
By Pascal Kadushi



