Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt. Doto Mashaka Biteko ameuagiza Uongozi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mufindi kuhakikisha Zahanati ya Kijiji cha Mkangwe, iliyounganishiwa umeme wa REA inaanza kazi mara moja.
Ametoa maagizo hayo leo, Februari 22, 2024 wakati akizungumza na wananchi baada ya kuwasha umeme katika Zahanati hiyo.
“Umeme tayari tumewasha, kwahivyo hakuna haja ya kusubiri. Naagiza Zahanati hii ianze kazi Jumatatu ijayo (Februari 26) ili wananchi wapate huduma za afya kama Serikali ilivyodhamiria,” amesisitiza.
Aidha, Dkt. Biteko amewaagiza Wakandarasi wanaotekeleza miradi ya umeme vijijini nchini kote kuhakikisha wanakamilisha kwa wakati ili Serikali iendeleze miradi hiyo katika maeneo mengine ambayo hayajafikiwa.
Amesema kuwa kadri miradi ya umeme vijijini inavyoendelea kutekelezwa katika maeneo mbalimbali, kiu ya wananchi ambao hawajafikiwa inaongezeka hivyo ameiagiza REA kuhakikisha inasimamia suala la ukamilishwaji miradi hiyo kwa wakati.
Awali, akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa miradi ya umeme vijijini kwa Mkoa wa Iringa, Mwakilishi wa Mkurugenzi Mkuu wa REA, Mhandisi Godfrey Chibulunje amesema kuwa Vijiji vyote 360 vya Mkoa huo, sawa na asilimia 100 vimepatiwa huduma ya umeme kupitia miradi mbalimbali inayotekelezwa na Wakala wa Nishati Vijijini (REA).
Na Pascal Kadushi


