AFUNGWA MIAKA 30 KWA KUTUMIA SILAHA KU NYANG'ANYA

 


Mkazi wa Kijiji cha Bugolola wilayani Ukerewe mkoani Mwanza, John Chibuga (31) amehukumiwa kifungo cha miaka 30 jela baada ya kutiwa hatiani kwa unyang'anyi wa kutumia silaha.

 

Hukumu hiyo imetolewa jana Februari 22.2024 na Hakimu Mkazi Mwandamizi wa  Mahakama ya wilaya ya Ukerewe, Lucas Nyahega ambapo amesema kupitia ushahidi uliotolewa mahakamani hapo, Mahakama imejiridhisha pasi na shaka kwamba mshtakiwa ametenda kosa hilo na hivyo inamhukumu miaka 30 jela.

 

Awali, akisoma shtaka hilo, Mwendesha Mashitaka wa Serikali, Aidan Nziku alisema mshtakiwa alitenda kosa hilo tarehe 15.12.2023 muda wa saa 14:00 mchana katika kijiji cha Kakerege wilaya  ya  Ukerewe kwa kumvamia  Mdala Mangu ( 34) akiwa Nyumbani kwake na kumkata na panga sehemu mbalimbali ya mwili wake kisha kuiba simu ya mkononi na kukimbia kinyume na kifungu namba 287A cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu sura 16 toleo la mwaka 2022.

 

Hata hivyo, mshitakiwa alipopewa nafasi ya kujitetea ili apunguziwe adhabu kutokana na shitaka linalomkabili,aliomba mahakama impunguzia adhabu kwa sababu alikuwa hana pesa ya kujikimu baada ya kutoka gerezani ndio akaamua kwenda kupora.

 

Aidha, Mwendesha mashtaka aliiambia mahakama  kuwa mshitakiwa ni mtenda kosa wa mara ya pili na aliachiliwa huru kwa msamaha wa Mhe. Rais tarehe 09.12.2023 kwa kosa la Kuvunja Duka Usiku na kuiba ambapo alitiwa hatiani na mahakama ya Mwanzo Nansio  na tarehe 15.12.2023 akarudia kutenda kosa.

 

Ili iwe fundisho kwake na onyo kwa jamii hususani wafungwa wanaoachiwa huru kwa msamaha wa Mheshimiwa Rais mwendesha mashtaka ameiomba mahakama hiyo itoe adhabu kali.

 

Kutoka Dawati la Habari Polisi Mwanza

By Pascal Kadushi

Post a Comment (0)
Previous Post Next Post