MWANZA.POLISI YAKAMATA WATUHUMIWA 98, WATUHUMIWA 6 KWA HUJUMA ZA MIUNDOMBINU YA UMEME

 

Hali ya usalama katika Mkoa wa Mwanza ni shwari, huku Jeshi la Polisi likiendelea kuimarisha ulinzi na usalama kwa kufanya doria na operesheni mbalimbali za kukabiliana na uhalifu. 

Jeshi hilo pia limeendelea kutoa elimu kwa wananchi kuhusu ushirikishwaji wa jamii katika kuzuia na kutanzua uhalifu, pamoja na kusikiliza na kufanyia kazi changamoto za kiusalama kupitia mikutano inayofanywa na Kamanda wa Polisi Mkoa, wakuu wa polisi wilaya, maafisa wa madawati ya uelimishaji na wakaguzi wa kata. Kupitia utaratibu huo, jumla ya wananchi 120,000 wamepatiwa elimu, huku changamoto zilizobainishwa na taarifa kutoka vyanzo vya kiintelijensia zikisaidia kupanga doria na operesheni za kiusalama.




Katika operesheni iliyoanza Oktoba 1, 2026, Jeshi la Polisi limewakamata watuhumiwa 98 kwa tuhuma za makosa mbalimbali ya jinai, yakiwemo kuhujumu miundombinu ya TANESCO, uvunjaji wa nyumba usiku na mchana, wizi, kupatikana na pombe ya moshi pamoja na mitambo yake, kukiuka masharti ya leseni za biashara na kupatikana na dawa za kulevya. 


Operesheni hiyo pia imewezesha kukamatwa kwa mali mbalimbali zinazohusishwa na matukio ya wizi, zikiwemo vifaa vya miundombinu ya umeme na mawasiliano: Polymeric 4, High Nuts 36, Tension Clamp 24, Distance Nail 8, Mid Span Joint 30, Fish 100 na vipande vya nyaya za umeme vyenye urefu wa mita 150, ambavyo baadhi ya wamiliki wamevitambua. Watuhumiwa sita wanaotuhumiwa kuhujumu miundombinu wanaendelea kuhojiwa na wanatarajiwa kufikishwa mahakamani kwa hatua zaidi za kisheria.

Post a Comment (0)
Previous Post Next Post