SOYA ONE LIMITED YATUNUKIWA TUZO YA HESHIMA KANDA YA ZIWA, YAANDIKA HISTORIA MPYA MARA

 

Kampuni ya Soya One Limited imeandika historia mpya baada ya kutunukiwa Tuzo ya Heshima Mdau Shupavu Kanda ya Ziwa katika sekta ya madini mkoani Mara. Tuzo hiyo imetolewa na Holysmile kwa kutambua mchango mkubwa wa kampuni hiyo katika maendeleo ya jamii na kukuza sekta ya madini ndani ya Mkoa wa Mara na Tanzania kwa ujumla.

Hafla ya utoaji wa tuzo hiyo imefanyika katika ukumbi wa Golden Crest Hotel, ikihudhuriwa na viongozi mbalimbali, wadau wa sekta ya madini pamoja na wageni mashuhuri kutoka ndani na nje ya mkoa.



Akizungumza katika hafla hiyo, Mkurugenzi wa Holysmile, Bweichum, ameipongeza Soya One Limited kwa kuwa mfano wa kuigwa katika uwajibikaji wa kijamii. Amesema kampuni hiyo imeonesha vitendo halisi vya kuunga mkono maendeleo ya jamii, kusaidia makundi mbalimbali na kushiriki kikamilifu katika ustawi wa wananchi.



Kwa upande wake, Mwakilishi wa Soya One Limited na Afisa Habari wa kampuni hiyo, Daniel Mussa, amesema tuzo hiyo ni heshima kubwa kwa kampuni na ni uthibitisho kuwa juhudi zao zinatambuliwa. Ameeleza kuwa kupitia kauli mbiu yao ya “Jamii Kwanza,” kampuni itaendelea kusimamia misingi ya uwazi, uwajibikaji na kuchangia maendeleo ya kijamii kwa vitendo.

Aidha, ametoa wito kwa wawekezaji na wageni kuutembelea Mkoa wa Mara kwa uwekezaji na utalii, akisisitiza kuwa ni mkoa salama, safi na wenye fursa nyingi za kiuchumi. Pia amewakaribisha wawekezaji kufika Wilaya ya Tarime, akieleza kuwa ni eneo lenye amani, rasilimali na mazingira rafiki kwa uwekezaji.



Kupitia tuzo hii, Soya One Limited imeendelea kuthibitisha nafasi yake kama mdau muhimu wa maendeleo, ikiweka mbele maslahi ya jamii na kuchochea ustawi wa uchumi wa Mkoa wa Mara na Taifa kwa ujumla.

Post a Comment (0)
Previous Post Next Post