MAPINDUZI YA AJIRA: PIKIPIKI 12,000 ZA UMEME KWA VIJANA ILEMELA


Mawaziri wawili; Deus Sangu na Joel Nanauka, leo Ijumaa Februari 20,2026 wameshuhudia utiaji saini mkataba wa ushirikiano baina ya Kafiti Foundation na kampuni ya ENERSCI & CHAJA AFRICA LTD juu ya utekelezaji wa  mpango mkubwa wa kukopesha pikipiki 12,000 kwa vijana wa jimbo la Ilemela mkoani Mwanza kwa masharti nafuu na rafiki.


Akizungumza wakati wa  ufunguzi wa mradi wa mafunzo ya kuwajengea ujuzi madereva wa pikipiki na bajaji 470 wa wilaya ya Ilemela, uliofanyika katika viwanja vya chuo cha VETA Nyakato, mbunge wa jimbo la Ilemela Kafiti William Kafiti amesema

lengo la pikipiki za umeme ni kupunguza hewa ukaa, kusaidia vijana kiuchumi na kufungua fursa za ajira.


Amesema mradi wa pikipiki hizo za umeme, utatekelezwa sambamba na uwekaji wa vituo vya kuchaji pikipiki za umeme katika maeneo mbalimbali ya Ilemela ili kurahisisha huduma, kupunguza gharama za uendeshaji na kuongeza faida, hatua aliyosema inalenga kupanua wigo wa ajira kwa  vijana.


Katika hatua nyingine, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais - Maendeleo ya Vijana Joel Nanauka ameishauri jamii kutowabeza vijana wanaojihusisha na shughuli za usafirishaji kwani ni kazi halali inayotambuliwa na Serikali na ajira hizo zitaendelea kuwekewa mikakati ili itengenezwe kuwa ajira rasmi.


Kwa upande wake, Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Ajira na Mahusiano Deus Sangu amesema Serikali ya Awamu ya Sita kuanzia Novemba 2025 hadi Kufikia Februari 18, 2026, vijana 2,348 wamepelekwa kufanya kazi zenye staha nje ya nchi, huku akitangaza fursa za vijana zaidi ya 500 wa bodaboda wanaotakiwa kwenda kufanya kazi katika nchi za Falme za Kiarabu - Dubai na wengine 1,150 watapelekwa na Serikali nchini Qatar kwa ajili ya kuendesha mabasi na magari makubwa ya mizigo.



Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – Maendeleo ya Vijana, Mhe. Joel Nanauka (Mb), akiwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Ajira na Mahusiano, Mhe. Deus Sangu (Mb), pamoja na Mbunge wa Jimbo la Ilemela, Mhe. Kafiti William Kafiti, wakiwasili eneo la Chuo cha VETA Nyakato, jijini Mwanza, kushiriki katika hafla ya ufunguzi wa mafunzo ya udereva pikipiki na bajaji, tarehe 20 Februari, 2026.






Post a Comment (0)
Previous Post Next Post