Jeshi la Polisi Mwanza Laanza Uchunguzi wa Wizi wa Mtoto Mchanga wa Siku Moja Buzuruga Mwanza

 

 

Jeshi la Polisi Mkoa wa Mwanza, linatoa taarifa kuhusu tukio la wizi wa mtoto mchanga mwenye umri wa siku moja lililotokea tarehe 07/02/2026 majira ya saa 16:00hrs huko Buzuruga, wilaya ya Ilemela jijini Mwanza.

 

Kwamba mnamo tarehe 06/02/2026 majira ya 18:00hrs mwanamke aitwaye NICE AJUNA RENATUS miaka 24, mkazi wa mtaa wa Nyasaka Msumbiji, alifika katika kituo cha afya Buzuruga kujifungua. Mwanamke huyo alijifungua salama mtoto wa jinsia ya kike na kupewa mapumziko katika chumba namba 4 kwenye zahanati hiyo.  

Akiwa amepumzika ndipo alifika mwanamke jina halijafahamika umri wake unakadiriwa kuwa kati ya miaka 35 au 40 nakujitambulisha kuwa ni mke wa mjomba wake na alifika kwa ajili ya kumuona, mwanamke huyo alitoa huduma mbalimbali ikiwa ni pamoja na kumpatia chai.

 

Ilipofika tarehe 07/02/2026 majira ya 17:00hrs NICE AJUNA RENATUS akiwa na kichanga chake cha siku moja aliruhusiwa kutoka hospitali baada ya hali yake ya kiafya kuwa sawa na wakati  anaondoka hospitalini hapo kuelekea nyumbani ndipo mwanamke aliyejitambulisha kuwa ni mke wa mjomba wake alimuomba amsaidie kubeba mtoto ili waelekee nyumbani, wakiwa njiani alimpitisha vichochoroni hadi kwenye nyumba ambayo alidai kuwa ni nyumba yake. Alizunguka nyumba akidai anatafuta funguo ili waingie ndani kisha akatoweka na mtoto kusikojulikana. 

 

Mama mzazi wa mtoto alibaki nje ya nyumba hiyo hadi alipoanza kutiliwa wasiwasi na familia ambao ni wamiliki halali wa nyumba hiyo ndipo ikabainika kuwa, mama huyo alikuwa ameibiwa mtoto wake mwenye umri wa siku moja na taarifa kufikishwa kituo cha Polisi.

 

Jeshi la Polisi Mkoa wa Mwanza, linaendelea kufanya uchunguzi wa kina kuhusiana na tukio hilo ili kubaini chanzo cha tukio hilo na kumkamata mwanamke huyo ambaye amefanya tukio la wizi wa mtoto.  

Aidha, Jeshi la Polisi linatoa wito kwa wananchi wa Mkoa wa Mwanza hususani akina mama kuchukua tahadhari za kutosha na kuacha tabia za kuamini watu wasiowafahamu na kuwakabidhi watoto ili wawashikie badala yake wasaidiwe na watu, ndugu, jamaa na marafiki wanaowafahamu. Mtu yeyote mwenye taarifa zinazoweza kusaidia kukamatwa kwa mtuhumiwa huyo na kupatikana kwa mtoto asisite kuziwasilisha kituo chochote cha Polisi kwa hatua zaidi.

 

 


Post a Comment (0)
Previous Post Next Post