Katibu Tawala Mkoa wa Mwanza Ndugu Balandya Elikana ametoa wito kwa Wizara inayoshughulikia vijana kushirikiana na sekta mtambuka kama SIDO na TEMDO kuhakikisha wanaliingiza kundi hilo katika uzalishaji unaotumia teknolojia ya kisasa.
Ametoa wito huo mapema leo tarehe 17 Februari, 2026 ofisini kwake wakati alipowapokea na kuzungumza na ugeni kutoka Ofisi ya Rais Maendeleo ya Vijana waliopo Mkoani humo kwa ziara ya kikazi.
“Nyie kama Wizara mnaoshughulikia vijana muna wajibu wa kuhusisha sekta zingine ili kubaini kama kuna miundombinu, mitaji au teknolojia rahisi za kukuza ubunifu wao ili kuhakikisha makundi ya ujasiriamali wanajiajiri kwa kutumia fursa zilizopo na kuleta tija.” Ndugu Elikana.
Aidha, ametoa rai kwa wizara hiyo kuangalia namna ya
kuwaingiza vijana kwenye ajira zisizo rasmi kwa kuwaingiza kwenye ufugaji,
kilimo na viwanda kama vya kutengeneza vyakula vya mifugo na kukuzia vifaranga
vya samaki ili kulitoa taifa kwenye changamoto ya ajira kwa vijana.
Bw. Edward Haule, Mkurugenzi wa ufuatiliaji na tathmini na mratibu wa mfuko wa
Maendeleo ya Vijana kutoka Wizara ya Maendeleo ya Vijana amesema Wizara
imejipanga vema kuhakikisha kundi hilo muhimu kwa maendeleo ya taifa linapata
ajira.
Ameongeza kuwa wizara inahakikisha kuwa vijana wanakuwa na shughuli endelevu
zinazozalisha kipato na ajira kwa wengine na katika kufanikisha hayo Wizara itaandaa
Mazingira wezeshi ya kimiundombinu na mitaji sambamba na kuhusisha taasisi
binafsi.
Aidha, amewataka Vijana kuhamasika na kutumia fursa hiyo kwa kuanzisha Miradi
yenye tija kulingana na rasilimali zinazopatikana kwenye Mazingira yao ili
waweze kujumuishwa kwa urahisi kwenye programu za maendeleo.






