Mwanza, Januari 27, 2026 – Katika maadhimisho ya siku ya kuzaliwa ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Mkoa wa Mwanza umeungana na wananchi kupanda miti 12,758 katika maeneo mbalimbali, tukio lililoratibiwa kwa ushirikiano na Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS).
Hayo yamebainishwa na Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Mhe. Said Mtanda, baada ya kushiriki zoezi la upandaji miti 1,200 katika Shule Mpya ya Sekondari Kakebe-Igoma, wilayani Nyamagana, akihitimisha zoezi lililoanza katika Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Ilemela.
“Mkoa wa Mwanza umeungana na Mheshimiwa Rais kufanya kazi za kijamii kwa kupanda miti ya matunda, ili kuunga mkono lishe bora kwa watoto wa siku za baadaye na kusaidia uhifadhi wa mazingira. Napenda kuwataka wananchi kupanda miti katika mashamba na kaya, si tu kwa ajili ya kivuli, bali kama sadaka ya kujenga taifa la kijani,” alisema Mtanda.
Aidha, Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana, Mhe. Amina Makilagi, alisema zoezi hilo limehamasisha upandaji miti katika maeneo yote ya wilaya, ikiwemo kaya za wananchi, huku wakipanda miti ya matunda ili kuchangia lishe bora na mazingira bora.
Hafla hiyo pia ilitumika kushukuru Serikali kwa kuleta fedha za miradi ya maendeleo, ikiwemo Tshs. 1,800,000 zilizokusanywa kupitia harambee kuunganisha umeme na maji katika shule hiyo mpya. Sehemu ya fedha Tshs. 1,350,800 ilipatikana papo hapo, na Meneja wa TANESCO ameagizwa kupeleka umeme mara moja huku maji yakifuata kwa kushirikiana na Mkurugenzi wa Jiji.
Meneja wa Kanda ya Ziwa wa TFS, Ebrantino Mgiye, alisema
wakala huo umeendelea kushirikiana na ofisi za mkoa na wilaya kutoa miche,
elimu ya uhifadhi wa misitu, na ushauri wa kitaalamu kwa wananchi na shule,
kuhakikisha miti inayopandwa inatunzwa na kudumu.
“TFS inashirikiana na jamii kuhakikisha zoezi hili linatekelezwa kwa usahihi,
miti inatunzwa, na wananchi wanapata elimu na ushauri wa kitaalamu wa uhifadhi
wa mazingira,” alisema Mgiye

.jpg)
.jpg)
.jpg)
.jpg)
.jpg)
.jpg)