ZAIDI YA MITUNGI YA GESI 1,500 YATOLEWA KWA BEI YA RUZUKU BUKOMBE

 

Wananchi wametakiwa kuunga mkono jitihada za Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan za kutumia Nishati Safi ya Kupikia ili kuimarisha afya zao sambamba na kutunza mazingira.


Wito huo umetolewa Oktoba 10, 2024 Wilayani Bukombe na Mkurugenzi wa Teknolojia za Nishati Jadidifu na Mbadala kutoka Wakala wa Nishati Vijijini (REA), Mhandisi Advera Mwijage wakati wa Semina maalum ya Nishati  Safi ya Kupikia kwa wakazi wa Wilaya hiyo.


"Rais wetu Dkt. Samia Suluhu Hassan ni kinara wa ajenda ya nishati safi ya kupikia, anatupenda na anafanya kila njia kuhakikisha kila mwananchi anapata bidhaa za nishati safi za kupikia kwa gharama nafuu", alisema Mhandisi Advera.


Akizungumza wakati wa Semina hiyo, Mkuu wa Wilaya ya Bukombe, Mhe. Paskasi Muragili alimshukuru Rais Mhe. Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kutoa ruzuku kwenye bidhaa za nishati safi za kupikia suala ambalo alisema linakwenda kuimarisha afya za wananchi sanjari na kuhifadhi mazingira ambayo kwa kiasi kikubwa yameathiriwa na ukataji wa miti kwa ajili ya kuni na mkaa.


"Leo ni siku ya kihistoria kwa wakazi wa Bukombe, tunakwenda kupokea mitungi ya gesi kwa bei ya ruzuku na hizi ni jitihada za Dkt. Samia Suluhu Hassan na Serikali anayoiongoza," alisema Mhe. Muragili. 


Aliwaasa wananchi wote watakojipatia mitungi hiyo kuhakikisha inapomalizika wanajaza ili kuendelea kutumia nishati safi ya kupikia na si kurejea katika matumizi ya kuni na mkaa


Akizungumza wakati wa Semina hiyo, Mhandisi Mwijage alisema Wakala umepewa jukumu la kuhakikisha bidhaa za nishati safi za kupikia zinafika katika kila pembe ya nchi ili kumuwezesha kila mwananchi kuachana na matumizi ya nishati isiyo safi na salama.


"Serikali kupitia REA imetoa ruzuku kwa bidhaa zote za nishati safi za kupikia lengo ikiwa ni kuhakikisha hakuna mwananchi anaachwa nyuma," alisema.


Mhandisi Advera alisema kwa bidhaa za mitungi ya gesi (LPG) Serikali imeingia makubaliano na watoa huduma ya kusambaza mitungi na katika kila Wilaya ambapo kwa awamu hii kiasi cha mitungi 3,255 itatolewa kwa bei ya ruzuku katika kila Wilaya.


"Kwa hapa Bukombe, mtoa huduma atakayesambaza mitungi ni Kampuni ya Manjis ambapo mitungi hii ya kilo sita ikiwa kamili na vichomeo vyake itatolewa kwa shilingi 17,500 tu ambayo ni nusu bei," alisema Mhandisi Mwijage.


Semina hiyo imehudhuriwa na mamia ya wananchi kutoka pande mbalimbali za Wilaya ya Bukombe.


Post a Comment (0)
Previous Post Next Post