Nipo tayari kuimarisha uhusiano na Marekani "ikiwa watakuwa tayari" kufanya hivyo.Putin

 

Rais Putin amesema hayo alipokuwa akihitimisha mkutano wa siku tatu wa kundi la BRICS huko Kazan nchini Urusi mapema leo Ijumaa.

"Itategemea namna Marekani itakacvyouchukulia uhusiano baina yetu baada ya uchaguzi. Ikiwa watakuwa tayari, nasi tutakuwa tayari. Na ikiwa hawataki, basi ni sawa," Putin alisema katika mkutano na waandishi wa habari.

Uhusiano kati ya Urusi na Marekani umedorora kufuatia uvamizi wa Urusi nchini Ukraine mwaka 2022.

Lakini licha ya Urusi kutengwa kimataifa kutokana na uvamizi wake nchini Ukraine, kiongozi huyo wa Urusi Putin aliwakaribisha wawakilishi wa zaidi ya nchi 36 mjini Kazan wiki hii na kuwakutanisha wakuu wa nchi, ambao n pamoja na Waziri Mkuu wa India Narendra Modi na Rais wa China Xi Jinping.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres aliyekwenda Urusi na kukutana na Putin kwa mara ya kwanza katika kipindi cha zaidi ya miaka miwili, amemwambia kiongozi huyo kwamba kuna haja ya kupatikana "amani ya haki" kulingana na Mkataba wa Umoja wa Mataifa, sheria za kimataifa na maazimio ya Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa ili kumaliza vita nchini Ukraine.

Katibu Mkuu huyo alikutana na Putin pembezoni mwa mkutano huo wa BRICS, hatua iliyokosolewa vikali na Ukraine, iliyosema imekasirishwa kwa kuwa Guterres hakukubali mwaliko wa "mkutano wa Amani" wa Ukraine uliofanyika nchini Uswisi majira ya kiangazi.


Putin aidha alizishutumu nchi za Magharibi kwa kujaribu kuyakandamiza mataifa masikini na yanayoinukia kiviwanda kwa kuwawekea "vikwazo haramu vya upande mmoja,  ushawishi usio na kikomo wa kigeni kupitia kile wanachokielezea "kukuza demokrasia", haki za binadamu, na ajenda ya mabadiliko ya hali ya hewa."

Lengo moja kuu la mkutano huo lilikuwa ni kuongeza ushirikiano wa kiuchumi miongoni mwa wanachama wa BRICS, ikijumuisha njia mbadala za mifumo ya kifedha ambayo kwa sasa inatawaliwa na Magharibi.

"Lakini hatutengenezi mfumo wowote wa pamoja kwa sasa," Putin alisema. "Kile ambacho tayari tunacho kinatosha."

Post a Comment (0)
Previous Post Next Post