Chama Cha Ushirika wa Akiba na Mikopo cha Jeshi la Polisi nchini (URA SACCOS) kimepata mafanikio makubwa ikiwemo kupata tuzo mbalimbali za chama bora kwa miaka minne mtawaliwa.
Hayo yamejiri Oktoba 30,2024 jijini Mwanza wakati wa kufunga mkutano mkuu wa 16 wa Chama Cha Ushirika wa Akiba na Mikopo (URA Saccos) uliofungwa na Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi Mhe. Ally Gugu
Akizungumza na wawakilishi na watendaji wa URA SACCOS zaidi ya 200 waliotoka Tanzania bara na visiwani, Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi Mhe. Ally Gugu, ameyataja mafanikio ambayo chama kimefikia kuwa ni tuzo mbalimbali ambazo chama kimepata na kuwa chama bora cha ushirika wa akiba na mikopo sambamba na kupata hati safi mfulululizo kutoka kwa Mkaguzi wa nje.
"Mafanikio mengine ni kuongezeka kwa idadi ya wanachama kutoka wanachama 4,300 waliojiunga na Saccos hiyo mwaka 2006 hadi kufikia wanachama 48,001 hadi Septemba mwaka huu"
Aidha, hisa ya chama imeongezeka kutoka hisa zenye thamani ya Sh 17,026,693/= kwa mwaka 2006 wakati chama kilipoanzishwa hadi kufikia hisa zenye thamani ya Sh 13,116,632,826/= hadi Septemba mwaka huu.

Vilevile, bakaa ya akiba zenye thamani ya Sh 76,748,917/- kwa mwaka 2006 imeongezeka hadi kufikia bakaa ya akiba ya thamani ya Sh 114,633,882,815/= hadi Septemba 30 mwaka huu.
Kupitia taarifa yake Katibu Mkuu Mhe. Gugu, amesema tangu kuanzishwa kwa Chama hicho mwaka 2006 jumla ya mikopo 137, 871 yenye thamani ya Sh bilioni 561.7 ilikwishatolewa hadi kufikia Septemba 30, mwaka huu ambapo zaidi ya asilimia sabini na tano ya mikopo hiyo imetumika katika ujenzi wa makazi binafsi ya wanachama.
Kwa muktadha huo ni dhahiri kwamba kiasi hicho cha fedha kimeingia katika mzunguko wa fedha na kuchangia ukuaji wa pato ghafi (GDP) la Taifa na uchumi kwa ujumla na hivyo inaashiria kuwa sekta ya Ushirika nchini ikisimamiwa na kuimarishwa kwa weledi mkubwa inaimarika na kuwa miongoni mwa sekta zitakazoongoza katika ukuaji wa uchumi hapa nchini.
Katibu amesema kwa mwaka 2023 pekee Saccos iliwapatia wanachama wake faida ya kuweka akiba yenye thamani ya Sh bilioni 3.4 na msaada wa vifaa tiba wenye thamani ya zaidi ya Sh milioni 650 kwa hospitali, zahanati na vituo vya afya vya Jeshi la Polisi kwa mikoa yote nchini.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Bodi ya URA Saccos Kamishna wa Utawala na rasilimali watu CP Suzane Kaganda, ameishukuru serikali ya awamu ya sita chini ya uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt Samia Suluhu Hassan, kwa kuendelea kuboresha maslahi ya watumishi wa umma wakiwemo wa Jeshi la Polisi nchini.