Jeshi la Polisi mkoa wa Mwanza kwa kushirikiana na Jeshi la Magereza, Zimamoto na Uokoaji, Uhamiaji, Mgambo, Polisi Wasaidizi na klabu ya mazoezi ya Isamilo Jogging, leo Agosti 31, 2024 wamefanya matembezi ya hiari (route march) yenye lengo la kuweka utimamu wa mwili na kuimarisha ushirikiano wa taasisi hizo na wananchi.
Mazoezi hayo yamefanyika ikiwa ni mwendelezo wa mazoezi ya kujenga afya na kubadilishana uzoefu wa kushughulikia masuala mbalimbali ya kiutendaji wa vyombo vya ulinzi na usalama kutoka wizara ya mambo ya ndani ya nchi.
Akizungumza baada ya mazoezi hayo, mwenyekiti wa klabu ya Isamilo Jogging Abdulradhak Twaha amesema wamefarijika kushiriki katika mazoezi hayo ambayo yamejumuisha idara za wizara ya mambo ya ndani ya nchi ambayo yameshiriki katika matembezi hayo.
"Tunaona kwamba jeshi letu haliko mbali na raia kwa kutushirikisha kufanya hamasa kubwa ya mazoezi." Amesema Abdulradhak.
Kwa upande wake, Mrakibu Msaidizi wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji; Deus Ruta amesema mazoezi hayo ni mazuri na yanawaweka askari katika hali ya utayari na utimamu wa akili na mwili.
Naye Mkaguzi Msaidizi wa Jeshi la Magereza; Ramadhan Mgoyo amesema mazoezi yanasaidia pia katika afya ya akili hivyo ametoa ushauri kwa jamii kufanya mazoezi ili kukabiliana na tatizo la afya ya akili.
Sambama na hayo Afisa Mnadhimu wa Polisi mkoa wa Mwanza Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP) Gideon Msuya, amesema mazoezi siyo adhabu bali humsaidia mtu kuimarika kifikra na kufanya maamuzi sahihi kwa wakati sahihi.







