Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe. Said Mtanda leo amekutana na kufanya mazungumzo na Naibu Gavana kutoka Jimbo la Henan kutoka nchini China, Mhe. Liu Yujiang na kusema mahusiano baina ya Tanzania na China yamezidi kuwa na tija siku hadi siku.
Katika mazungumzo hayo yaliyofanyika leo Septemba 6, 2024 kwenye ukumbi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa ukiwajumuisha Menejiment kutoka pande zote mbili, Mhe. Mtanda amesema historia ya ushirikiano baina ya Mataifa hayo ni ya muda mrefu na ujio wao utazidi kukuza mahusiano kati ya Mwanza na Jimbo la Henan.
Naye Naibu Gavana Mhe.Liu Yujiang amesema licha ya Taifa lao kupiga hatua kubwa kiuchumi Duniani lakini wanajivunia uhusiano na Tanzania na utazidi kudumishwa ili kila upande unufaike katika nyanja zote za kimaendeleo
Waasisi wa muungano wa ushirikiano baina ya Mataifa hayo ni Rais wa awamu ya kwanza wa Tanzania, Hayati Julius Nyerere na Hayati Mao Tsetung kutoka China.
Na Mwandishi wetu Mwanza






