Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko ameshiriki katika Mkutano wa Kimataifa wa Hydrogen Barani Afrika unaoendelea nchini Namibia akimwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Mkutano huo unaohudhuriwa na washiriki zaidi ya 1000 kutoka ndani na nje ya Afrika, unajadili namna ya nchi za Afrika kushirikiana kuzalisha na kutumia Hydrogen ambayo ni nishati safi na salama kwa mazingira na kwa uchumi endelevu.
Akifungungua Mkutano huo Jijini Windhoek, Namibia, Makamu wa Rais wa Nchi hiyo, Mhe. Netumbo Nandi-Ndaitwah amewataka washiriki kutumia fursa ya mkutano huo kuainisha mbinu na mkakati unaoweza kutumika kuleta maendeleo ya nchi husika kwa kutumia rasilimali zilizopo.
Akitoa mfano wa Namibia, Makamu wa Rais amesema Namibia inajivunia matumizi ya Hydrogen kwa matumizi ya viwanda kwa manufaa nchi hiyo, nchi Jirani pamoja na mataifa mengine yaliyo katika mlengo wa matumizi ya nishati hiyo.
Aidha, amehimiza matumizi ya nishati safi kwa maendeleo ya nchi hizo huku akisisitiza ushirikishaji wa vijana kama nguzo muhimu ya maendeleo kwa bara la Afrika kutokana na mchango na uwezo wao kama nyenzo ya maendeleo katika nchi husika.
“Majadiliano haya ni muhimu yakazingatia ushirikishaji wa pande zote muhimu katika mkutano huu wa kimataifa ili kuwa na maendeleo ya kweli na endelevu kwa uchumi na maendeleo ya watu na nchi zao” amesema Mhe. Netumbo Nandi-Ndaitwah.
Awali katika majadiliano, Waziri wa Madini na Nishati wa Namibia Mhe. Tom Alweendo amesema wajumbe wa mkutano wanatakiwa kuzingatia kuwa nchi za Afrika na Washirika wake zinatakiwa kuzingatia kuwa matumizi ya rasilimali zilizopo yanahitaji ushirikiano badala ya ushindani.
Amesema Namibia imekuwa ikishirikiana na nchi nyingine barani Afrika katika matumizi rasilimali zilizopo na nchi nyingine washiriki zinakaribishwa kuunga mkono jitihada hizo ikiwemo uzalishaji na matumizi ya Hydrogen kwa ajili ya uzalishaji wa nishati safi ya kupikia na kuendesha shughuli za kiuchumi.
Na Pascal Kadushi






