Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania, Bw. Emmanuel Tutuba, amehudhuria mkutano wa 61 wa Kamati Tendaji ya Taasisi ya Usimamizi wa Uchumi na Fedha ya Afrika Mashariki na Kusini (MEFMI) uliofanyika Lilongwe nchini Malawi kuanzia tarehe 23 hadi 24, Agosti, 2024 katika Benki Kuu ya Malawi.
Mkutano huo uliwakutanisha Magavana wa Benki Kuu na watendaji wakuu kutoka taasisi za fedha za nchi wanachama wa MEFMI ambapo walijadili masuala mbalimbali ya kiuchumi na fedha.
Vilevile, wajumbe wa mkutano huu walijadili mabadiliko ya tabia nchi na athari zake katika utekelezaji wa majukumu ya Benki Kuu katika kusimamia uchumi na sekta ya fedha.
Aidha, Magavana hao walipata fursa ya kujadili usimamizi wa uchumi jumla kwa lengo la kuimarisha uwezo wa kuchambua na kutekeleza sera za uchumi kwa nchi wanachama.
Pia, Gavana alipata fursa ya kubadilishana uzoefu kuhusu mbinu, mikakati na changamoto mbalimbali zinazoikabili sekta ya uchumi na fedha kutoka kwa washiriki wengine wa mkutano huo.
Na Pascal Kadushi

