WAKUU WA SHULE SIMAMIENI MIRADI KWA WELEDI -NKWABI

 


Afisa Elimu Mkoa wa Mwanza, Martin Nkwabi amewataka wakuu wa shule za msingi nchini kusimamia kwa weledi miradi ya elimu inayotekelezwa katika shule zao kwani wao ndio wanukafaika wakubwa wa miradi ya hiyo.

Nkwabi ametoa rai hiyo leo Julai 9, 2024, mkoani Mwanza kwenye mafunzo ya wakuu wa shule za msingi na maafisa mazingira kuhusu miongozo mbalimbali inayotekelezwa kupitia program ya Uboreshaji wa Elimu ya Awali na Msingi (BOOST).

Amesema kupitia programu hiyo miundombinu ya madarasa imeboreshwa hali ambayo inapelekea kupungua kwa utoro wa wanafunzi, kupunguza changamoto ya kujua kusoma, kuhesabu na kuandika na kuongeza idadi ya uandikishaji wa wanafunzi na kusisitiza kuwa kunahitajika umakini katika usimamizi ili ulete mafanikio chanya kwa jamii.



“Programu ya BOOST inatusaidia walimu wakuu katika kutatua changamoto mbalimbali zilizokuwa zinatukabili ikiwemo utoro mashuleni, uandikishaji wa wanafunzi pamoja na wanafunzi kutokujua kusoma na kuandika hivyo vyote vikifanikiwa walimu mtakuwa mmefanikisha malengo ya serikali ya kuboresha elimu nchini."

Aidha, Nkwabi amewataka kuhakikisha wanazitumia siku tatu za mafunzo kwa umakini mkubwa kwa kuuliza maswali kuhusu mradi huo lengo kikiwa ni kuweza kutatua changamoto mbalimbali zilizojitokeza kwenye utekelezaji wa mradi awamu ya kwanza.

Pia amewataka maafisa mazingira kuhakikisha wanafanya ufuatiliaji wa miradi inayotekelezwa shuleni ili kubaini changamoto za mazingira kabla na baada ya utekelezaji wa mradi.

Mafunzo hayo yameshirikisha wakuu wa shule, maafisa mazingira kutoka mikoa ya Kagera, Tabora, Kigoma, Geita, Mara,Simiyu, Shinyanga na Mwanza.






Post a Comment (0)
Previous Post Next Post