MICHEZO INA NAFASI KUBWA YA KUTANGAZA UTALII: RC MTANDA

 

Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe. Said Mtanda ameshiriki mbio za kuhamasisha Utalii mkoani humo maarufu kama Transec Lake Victoria Marathon na akabainisha kuwa Michezo ni njia muhimu ya kutangaza na kukuza utalii ikiwemo vyakula vya kitamaduni.

Akizungumza leo Julai 7, 2024 kwenye uwanja wa Nyamagana mara baada ya kuhitimishwa Marathon hiyo ambayo naye ameshiriki, Mhe. Mtanda amesema Mwanza ina vivutio vingi vya utalii hivyo juhudi inayotakiwa sasa ni Jamii kuvitangaza ili viweze kujulikana ndani na nje ya nchi.


Aidha, amewapongeza waandaaji wa mbio hizo kwa ubunifu unaohitaji kuigwa pia wakimbiaji wote walioshiriki umbali tofauti kama Kilomita 21, 10, 5, na 2 na washindi kupata nishani na zawadi ya pesa zilizotolewa.

"Sekta ya utalii inachangia pato la Taifa kwa asilimia 17 kwenye GDP ya nchi vivyo hivyo inatoa ajira kwa watanzania zaidi ya milioni 1.6 hivyo ni sekta muhimu kwa Taifa letu", amesema Mkuu wa Mkoa.


Naye, Mkuu wa Kikosi cha usalama barabarani Mkoa wa Mwanza Sunday Peter amewashukuru wakimbiaji kwa kuwa na nidhamu na kufuata maelekezo wakati wa mbio hizo na kuwezesha kikosi cha usalama barabarani kufanya kazi yao kwa wepesi .

Kwa upande wake Rais wa Chama cha Riadha Tanzania Silas Wambura ametoa wito kwa wanamichezo kushiriki riadha zinazoandaliwa nchini ili kuwapata washiriki bora watakaoiwakilisha Tanzania katika medani za kimataifa.

Mbio hizo zilikuwa na lengo la kuhamasisha utalii wa ndani kanda ya ziwa pamoja na kuchangia taulo za kike kwa wasichana.

BAADHI YA PICHA MBALIMBALI KATIKA TUKIO HILI






Post a Comment (0)
Previous Post Next Post