KESI YA MSANI DITTO DHIDI YA DSTV YASOGEZWA MBELE

 

Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam imeahirishwa kwa mara nyingine kutoa hukumu ya kesi ya madai ya mwanamuziki Lameck Ditto dhidi ya kampuni ya Multchoice Tanzania Limited maarufu kama DStv.

Hukumu hiyo iliyopangwa kutolewa leo Jumaatu Julai 22, 2024 saa 4 asubuhi, imesogezwa mbele kwa siku moja hadi kesho saa 5 asubuhi. Hiyo ni mara ya pili kwa hukumu hiyo kuahirishwa, awali ilipangwa kutolewa Julai 16, 2024.

Hukumu hiyo sasa itatolewa kesho Julai 23, 2024 Mahakamani hapo mbele ya jaji mfawidhi, Salma Maghimbi.




Ditto ambaye jina lake halisi ni Dotto Bwakeya alifungua kesi ya madai mahakamani hapo mwaka 2020, akiiomba iamuru kampuni DStv imlipe fidia ya Sh6 bilioni kwa kutumia wimbo wa ‘Nchi Yangu’ aliodai ni wake kwenye matangazo yao ya biashara bila ridhaa yake wakati wa kampeni za fainali ya Mataifa ya Afrika (Afcon) mwaka 2019.

Pia ameiomba Mahakama iamuru alipwe Sh200 milioni kutokana na madhara ya jumla, pia alipwe riba ya asilimia 25 tangu siku alipofungua shauri hilo, akidai kampuni hiyo imemnyima fursa ya kunufaika na kazi yake.


Post a Comment (0)
Previous Post Next Post