Watu watatu wakiwemo walimu wawili wamefikishwa katika Mahakama ya Wilaya ya Kwimba Mkoani Mwanza Juni 20, 2024 na kusomewa mashtaka sita likiwemo la kutengeneza na kuwasilisha nyaraka za kughushi.
Mwendesha Mashtaka wa Serikali, Mkaguzi wa Polisi, Juma Kiparo amewataja washtakiwa hao kuwa ni mwalimu na Mkazi wa Vikindu mkoani Dar es Salaam, Benson William (33), Godfrey Cyprian (44), mfanya biashara ya steshenari na Mkazi wa Mtoni Unguja Wilaya ya Temeke na Mkoa wa Dar es salaam na Okeyo Otieno (36) mwalimu na Mkazi wa Kishiri Mkoani Mwanza ambapo wote wanashtakiwa katika Shauri la Jinai namba 16839/2024.
Akisoma mashtaka hayo mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi, John Chai Jagadi, Kiparo amesema washtakiwa wanadaiwa kutenda makosa hayo kwa nyakati tofauti kati ya Februari hadi Juni 10, 2024 Mkoani Mwanza na Dar es Salaam.
Mwendesha mashtaka amebainisha kuwa Februari 29, 2024 huko Wilaya ya Temeke Mkoa wa Dar es Salaam washtakiwa wote kwa pamoja walifanya kosa la kutengeneza barua ya kugushi uhamisho unaomhusu Tabu Bartholomew Maghonga ya kupandishwa cheo na kuwa Afisa Elimu Taaluma Idara ya Elimu Msingi yenye kumbu namba CCD 215/401/01M/8339 kwenda Mkoa wa Pwani Halmashauri ya Wilaya hiyo.
Pia ameieleza Mahakama kuwa April 09, 2024 huko maeneo ya Ngudu na Wilaya ya Kwimba Mkoani Mwanza washtakiwa wote watatu walifanya kosa la kuwasilisha barua ya kughushi yenye kumbu namba CCD 215/401/01M/8339 ya kupandishwa cheo na kuhama kwenda kwa Mkurugenzi wa Halmshauri ya Wilaya ya Kwimba inayomuhusu Tabu Bartholomew maghonga mtumishi wa umma anayefanya kazi Halmashauri ya Wilaya ya Kwimba.
Katika maelezo hayo, Kiparo amesema Machi 01, 2024 huko maeneo ya Tandika Wilaya ya Temeke Mkoa wa Dar es Salaam, washtakiwa wote watatu walighushi barua yenye kumbukumbu namba CCD 215/401/01M/8343 ya uhamisho wa Rutambi Mabala kutoka Wilaya ya Kwimba Mkoa wa Mwanza kwenda Wilaya ya Bariadi Mkoani Simiyu.
Pia, tarehe 09.06.2024 huko maeneo ya Ngudu Wilaya ya Kwimba na Mkoa wa Mwanza washtakiwa wote watatu waliwasilisha barua ya kughushi yenye kumbukumbu namba CCD 215/401/01M/8343 ya uhamisho wa Rutambi Mabala kwa Mkurugenzi wa Halmshauri ya Wilaya ya Kwimba.
Machi 19 2024 huko maeneo ya Tandika Wilaya ya Temeke na Mkoa wa Dar es salaam washtakiwa wote walifanya kosa la kutengeneza barua ya kughushi ya uhamisho inayomuhusu Yohana Shitungulu mtumishi wa serikali anayefanya kazi Halmashauri ya Wilaya ya Kwimba kuhamia Wilaya ya Temeke Mkoa wa Dar es salaam kutokea Wilaya ya Kwimba Mkoa wa Mwanza yenye kumbukumbu namba CCD 215/401/01S/8357.
April 09, 2024 huko maeneo ya Ngudu Wilaya ya Kwimba na Mkoa wa Mwanza watuhumiwa wote walifanya kosa la kughushi barua ya uhamisho wa Yohana Shitungulu kuwa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kwimba yenye kumbukumbu namba CCD 215/401/01S/8357.
Mwendesha Mashtaka huyo amesema washtakiwa wametenda makosa hayo kinyume na vifungu namba 333, 334,335(a), 337 na 342 vya Kanuni ya Adhabu Sura ya 16 ya Sheria marejeo ya mwaka 2022.
Hata hivyo, baada ya kusomewa mashtaka hayo, washtakiwa wote watatu wamekana mashtaka na kuiomba Mahakama kuwapatia dhamana kwani mashtaka yanayowakabili yanadhaminika.
Baada ya maelezo hayo, Hakimu Mkazi Mwandamizi wa Mahakama hiyo aliwataka washtakiwa kutimiza masharti ya dhamana ambayo ni kuwa na wadhamini wawili watakaosaini hundi ya maneno ya Sh. Milioni saba (7) kila mmoja na mmoja kati ya wadhamini alipaswa kuwa mtumishi wa serikali na kuwa na barua ya utambulisho kutoka kwa mwajiri.
Hata hivyo, mshtakiwa mmoja ameshindwa kutimiza masharti ya dhamana kwani hakuwa na wadhamini wawili waliokidhi matakwa ya dhamana.
"Mshtakiwa namba tatu kwa kuwa umeshindwa kutimiza masharti ya dhamana utakaa rumande hadi hapo utakapo weza kudhaminiwa" amesema Hakimu Jagadi.
Hakimu ameahirisha shauri hilo hadi Julai 2, mwaka huu litakapoitwa kwa ajili ya washtakiwa kuanza kusomewa hoja za awali.


