Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza Naibu Kamishina wa Polisi (DCP) Wilbrod Mutafungwa amewataka watendaji wa Kata kushirikiana na Polisi Kata kwenye maeneo yao ili kuzuia uhalifu.
Kamanda Mutafungwa ameyasema hayo Aprili 18, 2024 wakati alipotembelea Wilaya ya Kwimba kwa ajili ya ukaguzi ambapo alipata wasaa wa kuzungumza na Watendaji wa Kata zote pamoja na Polisi kata wilayani humo.
Akizungumza wakati wa kikao, Kamanda Mutafungwa amewaomba Watendaji hao ambao ni walinzi wa amani kushirikiana na Polisi Kata kutoa elimu kwa wananchi juu ya kuzuia uhalifu.
"Nimekuja kuwaomba watendaji wa kata mtusaidie kuelimisha wananchi kwa kushirikiana na Wakaguzi Kata kuhusu mambo ya kujichukulia Sheria mkononi ambayo yamesababisha mauaji katika maeneo yenu" amesema Kamanda Mutafungwa
"Jeshi la Polisi tunatamani kuona tunafanikiwa zaidi kuzuia uhalifu kuliko kupambana na uhalifu kwa sababu wote hapa mnaelewa namna ambavyo ni gharama kubwa kupambana na uhalifu na jinsi ambavyo ni gharama nafuu kuuzuia uhalifu" amesisitiza kamanda Mutafungwa
Kufuatia kikao hicho, Watendaji wa Kata wa Wilaya ya Kwimba wamempongeza Kamanda Mutafungwa kwa kuwapatia elimu ya pamoja na Wakaguzi Kata na kuahidi kuongeza ushirikiano zaidi kwa Jeshi la Polisi ili kidhibiti uhalifu katika maeneo yao
"Tunashukuru na tunapongeza ujio wa Kamanda Mutafungwa umetusaidia kupitia elimu na ushauri tunaenda kushirikiana na Polisi Kata katika vikao vya Vijiji na WDC, katika suala la ulinzi na amani ngazi ya Kata" amesema Mtendaji wa Kata ya Nyambiti Felister Mazinzi.
Katika hatua nyingine Kamanda Mutafungwa amekutana na Waganga wa tiba asilia pamoja na sungusungu na kuwataka kufanya kazi kwa kuzingatia sheria huku wakitenda haki pasipo kuleta chuki na uhasama katika jamii.


.jpeg)
.jpeg)