Mkurugenzi Mkuu wa wakala wa nishati vijijini Mhandisi, Hassan, Saidy amesema kuanza sasa kigezo kimojawapo kitakachotumika kuwapata Wakandarasi wanaotekeleza Miradi ya kusambaza nishati ya umeme vijijini ni taratibu zote za Sheria ya Ununuzi wa Umma pamoja na utendaji madhubuti (Performance) na si vinginevyo.
Mhandisi, Hassan Saidy ameyasema hayo wakati wa mkutano maalum kati ya REA na Wakandarasi wanaotekeleza Miradi mbalimbali ya kusambaza umeme vijijini, mkutano uliofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Julius Nyerere, Jijini, Dar es Salaam, Tarehe 13 Aprili, 2024.
Mhandisi, Saidy amesema mkutano huo maalum ulilenga mambo mbalimbali, moja ni kuwakumbusha Wakandarasi hao kuhusu wajibu wao wakati wa utekelezaji wa miradi ya nishati vijijini pamoja kujipanga kwa ajili ya kukamilisha Mradi mkubwa wa REA III (Mzunguko wa Pili) ambao unataraji kukamilika Mwezi Juni, 2024 ambapo imeelezwa kuwa vijiji vyote vimefikiwa na nishati ya umeme.
Mhandisi Saidy ameongeza kuwa mkutano huo pia, ulikuwa na lengo la kuwakumbusha kuhusu wajibu wao na nafasi zao kwenye Miradi ya usambazaji wa umeme vijijini na kuongeza kuwa pamoja na vigezo vya manunuzi ya zabuni kuwa vitazingatiwa ili kuwapata Wakandarasi watakaotekeleza Miradi hiyo, suala ya utendaji kazi bora, utakuwa kigezo muhimu kuanzia sasa.
“Tumewaambia kwamba ili Mkandarasi aweze kupata Mradi wa REA, pamoja na vigezo vyote vya Sheria ya Manunuzi ya Umma kuvifikia, lakini tutaangalia “performance” yake kwenye Miradi yetu, sisi wenyewe, kwa hiyo kama Mkandarasi atakuwa anasua sua na kufanya kazi vibaya, hatakuwa na nafasi ya kupata mkataba mwengine.” Amesisitiza, Mkurugenzi Mkuu.
Wakati huo huo, Viongozi wa Wakala wa Nishati Vijini wakiongozwa na Mwenyekiti wa Bodi ya Nishati Vijijini (REB); Mhe. Balozi na Meja Jenerali Mstaafu, Jacob Kingu walitumia mkutano huo kutoa nishani na vyeti maalum kwa Wakandarasi waliofanya vizuri.
Mhandisi Hassan Saidy amesema kuwa, REA iliamua kuwatunuku nishani na vyeti Wakandarasi wanaofanya vizuri kwenye usambazaji wa nishati ya umeme vijijini.
By Pascal Kadushi




