Wanafunzi mkoani Arusha wametakiwa kujenga tabia ya kushiriki michezo wawapo shuleni, kwa kuwa michezo huchangamsha mwili na akili ya binadamu, na kukuza uwezo wa huongeza uwezo wa kufikiri na kuchagiza ari ya kujifunza kwa mwanafunzi.
Rai hiyo, imetolewa na Mkuu wa mkoa wa Arusha Mhe. John V.K Mongella, wakati akikabidhi mipira 1000 ya Soka, iliyotolewa na Shirikisho la Mpira wa Miguu Duniani - FIFA, kupitia Chama cha Mpira wa Miguu Tanzania - TFF, kwa lengo la kuendeleza michezo shuleni, kuibua na kukuza vipaji vya wanafunzi wa shule za msingi na sekondari za mkoa huo.
Mhe. Mongella, amewasisitiza wanafunzi kushiriki michezo wawapo shuleni, kwa kuwa upo uhusiano mkubwa kati ya michezo na akili ya mwanafunzi katika uwezo wa kufikiri na kumuwezesha kufanya vizuri kwenye masomo licha ya kuwa michezo hujenga afya na pia ni ajira.
“Tunapaswa kutambua michezo ni afya, kila mmoja wetu ajenge tabia ya kushiriki michezo kwa kuwa huufanya mwili kuchangamka na kuondoa ugoigoi zaidi michezo huasha akili na kuongeza uwezo wa kufikiri hivyo kwa wanafunzi michezo huongeza na kuamsha uwezo wa kufujifunza, upo uhusiano chanya kati ya michezo na masomo” Amesisitiza Mkuu huyo wa Mkoa
Aidha, amewasisitiza Maofisa Elimu wa ngazi zote kwa kushirikiana na walimu kuwasimamia kutumia mipira hiyo kwa malengo yaliyokusudiwa ya kuendeleza soka shuleni pamoja na kuhakukisha wanafunzi wanashiriki michezo na kupata timu za kushiriki mashindano ya ngazi zote mpaka Taifa na Kimataifa


